skip to main |
skip to sidebar
CHADEMA YAMJIBU WAZIRI, YASEMA AMEDANGANYWA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga
kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye
kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na
askari Mkoani Morogoro na badala yake uchunguzi huru ufanyike haraka kwa
mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).
Kauli zilizotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani zina
mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo askari na maafisa wake ni
sehemu ya watuhumiwa wa mauaji badala ya kuwezesha ukweli kuthibitika na
hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
Hivyo kutokana na kujirudiarudia kwa mauaji
yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito Rais Jakaya
Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa nchi,
kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi
wa kina.
Ikumbukwe kwamba tarehe 27 Agosti 2012 Jeshi la
Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na kupiga mabomu ya
machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamejikusanya kwa
ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na kusababisha kifo
cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.
CHADEMA kinaukumbusha umma kwamba kwa mauaji hayo na
mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali inayoongozwa na CCM
kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka ibara ya 14 ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba uhai ni haki ya
msingi wa raia wote.
CHADEMA hakikubaliani na hatua zilizochukuliwa na
Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na maelezo yaliyotolewa
na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo kwa sehemu
kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maafisa wa Jeshi
la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.
CHADEMA haina imani na timu iliyoundwa na Mkuu wa
Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua risasi na mabomu ya
machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na jeshi la
polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na maelezo
ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.
Wakati Serikali na Jeshi la Polisi wakitoa maelezo
kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na kupelekwa hospitali na
wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari walifika jirani na
eneo lake na afisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi za moto na
mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na kudondoka.
Mashuhuda wote waliohojiwa wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo
ilielekezwa na kufyatuliwa kwa marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana
ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni bunduki ya risasi za moto na wengine wa
wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia mabomu ya machozi.
Mara baada ya kudondoka gari hilo liliondoka na gari
lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine kumbeba Ali Zona na
kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio hayo yalitokea mbali na
eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu na barabara ya
kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.
Kauli zilizotolewa na Serikali kuwa Jeshi la Polisi
lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa kufanyika Mkoani Morogoro
kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa kuwa sababu pekee
zilizotolewa na ufinyu wa barabara na kuwa maandamano yalipangwa siku ya
kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi lenyewe ya 23
Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA kinaujulisha umma kwamba Jeshi la Polisi
Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala wa sheria na
makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi kutoka
makao makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za
Jeshi hilo Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na
madhara mengine kwa wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya
machozi.
Ikumbukwe kwamba awali CHADEMA ilipanga kufanya
maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini tarehe 4 Agosti
2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, Polisi wakakataa kufanyika kwa maandamano
na mikutano kwa kisingizio cha sikukuu ya nane, mgomo wa walimu na
ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM sababu ambazo zilibainika
kwamba hazikuwa na msingi wowote.
Baada ya mvutano na mazungumzo CHADEMA ilikubali
kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la Polisi pamoja na kuwa
yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na mkutano wa CHADEMA
vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26 Agosti 2012
na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la Polisi
liliikubali.
Polisi walifanya hivyo wakielewa ukubwa wa barabara
za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni siku ya kazi, hata hivyo
tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi na kuandika barua ya kueleza
kwamba imetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake kisheria)
na pia ikakataza maandamano.
CHADEMA ikaamua kwa mara nyingine tena kurudi katika
meza ya mazungumzo mengine kati ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro
tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya
watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012
mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.
Hata hivyo, kufuatia shinikizo la Kamanda wa Polisi
wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume na Sheria ya Jeshi la
Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya kuhusu taarifa za
mikutano polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi ya
watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu
zenye misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba
ikapendekeza kwamba yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.
Maelezo ya Waziri wa Mambo ya Ndani iwapo vyama vya
siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa
yanapotosha kwa kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya
Siasa hazijaweka utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni
kutumia mahakama.
Jeshi la Polisi lingeheshimu utawala wa sheria na
mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa ulinzi mpaka
eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua kutumia
nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na
kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.
Iwapo wanachama na wananchi waliokuwa wamekusanyika
kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano wangekuwa wamekiuka sheria
Jeshi la Polisi lingeweza kuwamata kwa mujibu wa sheria, hata hivyo
hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada mpaka sasa
katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.
Kinyume chake Jeshi la Polisi ambalo lilikuwa kwenye
mazungumzo limekubali kuwa mapokezi yafanyike kwa kwa msafara wa vyombo
vya usafiri tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu ya machozi kwa
wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la Msamvu
wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika
matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na
vyombo vingine vya usafiri.
Kitendo cha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa
kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga barabara kwa muda
mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla
kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani
kutembea kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona
wamesababisha hali hiyo wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la
mkutano hali inayodhihirisha kuwa uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka
mwanzo yasingetokea madhara yoyote.
Kwa kuzingatia utofauti mkubwa baina ya maelezo
yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu matukio husika na
ukweli halisi ulivyotokea CHADEMA kinasisitiza kuwa uchunguzi huru
ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya
24 ya Sheria za Tanzania.
CHADEMA kwa mara nyingine kinaitaka Serikali
inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3 cha Sheria hiyo ambacho
kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha
Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo (Coroner’s Court) katika maeneo ya
serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji Kiongozi.
CHADEMA kinaikumbusha Serikali kuwa iliahidi bungeni
kufuatia Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mawaziri vivuli
husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola
kwa nyakati mbalimbali Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi kwamba
sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata hivyo katika
muktadha huo uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya
polisi bali sheria hiyo sasa ianze kutumika.
Kwa upande mwingine, CHADEMA imeheshimu taratibu za
maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa marehemu ulisafirishwa
jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili ya maziko na
CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu
ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano
yanayoendelea na familia.
CHADEMA kwa kuheshimu mazungumzo na utawala wa sheria
kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA kimesitisha
Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko
(M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) kupitisha
kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka
zingine za kiserikali.
CHADEMA inatambua kwamba wakati maandamano ya CHADEMA
yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa, maandamano ya wagombea wa
CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao yameachwa
yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio
hicho.
Aidha, wakati CHADEMA ikiheshimu mazungumzo na
kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012 mpaka tarehe 27
Agosti 2012 kupitisha Sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya
tarehe hiyo.
Tume hiyo inaendelea na mikutano yake ya hadhara
inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa mbalimbali wakati huo huo
zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya CHADEMA inaonekana
kufanyika kwake ni kuingilia sensa.
CHADEMA inataka Serikali na Polisi kueleza iwapo
matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na uhujumu wa
vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli kuwa
maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa
maslahi ya wengi.
CHADEMA itaeleza hatua za ziada itakazochukua baada
ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu (post mortem)
uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali au
kukataa mwito wa kutumia sheria ya Vifo (Inquest Act) kuwezesha
uchunguzi huru.
Imetolewa tarehe 29 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi
JIUNGE NA EDMO BLOG SASA
Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube
Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi