Ndugu
Waandishi wa Habari,
Ndugu Wananchi, kama
tunavyofahamu kwamba Meli ya MV. SKAGIT iliyokuwa ikifanya safari
kutoka Dar es Salaam kuja Zanzibar tarehe 18 Julai, 2012 ilipata ajali
katika eneo la karibu na Kisiwa cha Chumbe na kupelekea meli hiyo
kuzama. Meli hiyo ilitengenezwa nchini Marekani mwaka 1989 na
imesajiliwa Zanzibar tarehe 25 Oktoba, 2011 na kupewa nambari ya Usajili
100144, yenye uzito wa GRT96. Kampuni inayomiliki meli hiyo ni Seagull
Sea Transport Limited ya Zanzibar.
Meli hiyo kikawaida inafanya safari zake baina ya visiwa vya
Unguja na Pemba na Dar es Salaam. Siku hiyo ya tarehe 18 Julai, 2012
meli hiyo iliondoka Dar es Salaam majira ya saa 6.00 mchana kuelekea
Zanzibar. Kwa mujibu wa Manifest ya abiria iliowasilishwa na wenye meli
kwa mamlaka husika (TPA na SUMATRA), meli hiyo ilikuwa imechukua watu
290 kwa mchanganuo ufuatao:-
1. Abiria watu wazima - 250
2. Watoto - 31
3. Mabaharia - 9
Mnamo saa 7.30 mchana meli hiyo ilizama karibu na eneo la
Kisiwa cha Chumbe takriban umbali wa maili 7 za baharini kufikia kisiwa
hicho.
Ndugu Wananchi, Serikali kupitia vyombo
vyake vya Bandari, ZMA na Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Kampuni
Binafsi vilianza kuchukua hatua ya kwenda katika eneo la tukio kwa
ajili ya kutoa huduma za uokozi. Mnamo majira ya saa 9.15 harakati za
uokozi zilianza kwa kuokoa wananchi waliokuwa hai na baadae kuanza
zoezi la kutafuta maiti.
Vyombo vingi vilishiriki kikamilifu katika jitihada za uokozi,
ikiwemo Kilimanjaro 3, Tagi ya Bandari, Flying Horse, Helikopta za
Jeshi la Wananchi na Polisi, Zanzibar One, Boti za KMKM ambazo pia
zilikuwa na wazamiaji (divers).
Ndugu Wananchi, katika jitihada hizo jumla ya watu 146
waliokolewa wakiwa hai. Hadi kufikia jana jioni maiti zilizopatikana
zilifikia 73, wakiwa wanaume 19, watoto 17 na wanawake 37. Kwa ujumla
maiti nyingi zilitambuliwa na kukabidhiwa jamaa zao kwa ajili ya
mazishi. Serikali iligharamia mazishi hayo kwa kutoa vifaa vya kuzikia.
Jumla ya maiti 23 hazikuweza kutambuliwa na jamaa zao na hivyo
iliamuliwa kuzikwa na Serikali katika makaburi ya Kama nje kidogo ya
mji wa Zanzibar ili kuepuka kukaa zaidi na maiti hizo kuharibika.
Jitihada zaidi zinaendelea kuchukuliwa na Serikali kutafuta miili
iliyokuwa haijaonekana. Hata hivyo, kwa wakati huu imeamulika maiti
zitakazopatikana kuanzia sasa zitapelekwa moja kwa moja katika eneo la
Kama kwa ajili ya mazishi. Kutokana na hali hiyo na baada ya Masheikh
kutoa Fat-wa, iliamuliwa kufungwa kwa kambi ya Maisara iliyokuwa
ikitumika kwa ajili ya utambuzi wa maiti.
Ndugu Wananchi, kwa taarifa tulizonazo, miongoni mwa abiria
waliokuwa katika chombo hicho, walikuwemo raia wa kigeni 17 na
waliookolewa wakiwa hai 15, mmoja amepatikana akiwa amefariki na mmoja
hajapatikana hadi sasa. Wageni hao ni kutoka Ubelgiji, Marekani,
Ujerumani, Uholanzi na Israel. Serikali ilitoa huduma kwa wageni hao na
tayari wameondoka kurudi makwao kwa salama.
Ndugu Wananchi, jitihada za kukitafuta chombo kilichozama
zilifanyika kwa kutumia wataalamu wa uzamiaji kutoka Kikosi cha KMKM,
Jeshi la Wananchi, Polisi pamoja na wazamiaji wa kujitolea wa Ki-Israel
ambao wapo Nungwi. Wazamiaji wetu hawa walifika umbali wa mita 48
chini ya bahari lakini kwa bahati mbaya hawakuweza kuiona meli hiyo.
Hata hivyo, jitihada zinaendelea.
Ndugu Wananchi, nachukua fursa hii kuwaomba wananchi wote
wanaoishi katika maeneo ya mwambao na wanaofanya shughuli zao katika
maeneo ya baharini watoe taarifa kwa Serikali katika maeneo yao pale
wanapoona miili ya watu wanaosadikiwa kuwa ni abiria wa meli iliyozama.
Aidha, wananchi wote waliopotelewa na jamaa zao ambao wanadhani
walikuwa katika chombo hicho kutoa taarifa kwa masheha na wakuu wa
wilaya au Vituo vya Polisi vilivyo karibu nao.
Ndugu Wananchi, Kati ya majeruhi 138 waliopelekwa hospitali ya
Mnazi Mmoja hadi kufikia leo hii wagonjwa wote walikwisha ruhusiwa
baada ya kupata matibabu katika hospitali.
Ndugu Wananchi, Serikali imehuzunishwa sana na tukio hili na
imekusidia kuchukua hatua mbali mbali, ikiwemo kutoa mkono wa pole kwa
wahusika na kuunda Tume ya Uchunguzi wa ajali hii. Aidha, Serikali
iliagiza Mikoa yote kusoma hitma na dua za kuwaombea marehemu na
waliopatwa na ajali hii.
Katika hatua ya kudhibiti majanga ya aina hii, Serikali
inakusudia kuzifanyia mapitio sheria zinazohusu usafiri wa baharini na
kuweka viwango vya aina ya meli zitakazoruhusiwa kuingizwa nchini na
kuchukua abiria. Aidha, Serikali inakusudia kuendelea na juhudi zake za
kununua meli zake kwa ajili ya kutoa huduma za usafiri wa hakika kwa
wananchi katika maeneo ya mwambao.
Ndugu Wananchi, napenda kuchukua nafasi hii kuyashukuru sana
Makampuni binafsi na vyombo vya usafiri wa baharini kwa msaada na
ushirikiano mkubwa waliotupa kuanzia mwanzo wa zoezi hili hadi mwisho.
Lakini pia napenda kuzipongeza Kamati zetu za Maafa za Tanzania Bara
kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu na ile ya Zanzibar kutoka Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais kwa kufanya kazi kwa pamoja kusimamia zoezi hili la
uokozi.
Ndugu Wananchi, napenda pia kuwashukuru wananchi wote wa
Zanzibar na Tanzania kwa jumla wakiwemo wafanyabiashara mbali mbali kwa
misaada yao mbali mbali walioitoa na vyombo vya habari kwa ushirikiano
wao wakati wote wa tukio hili ambapo walikuwa wanawajulisha wananchi
wetu hali inavyoendelea.
Vile vile, napenda kuwashukuru Viongozi wetu wakuu kwa
ushirikiano wao mkubwa waliotupa katika maafa haya. Ambao ni:- Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa namna alivyoliongoza zoezi zima la uokozi na kupata
mafanikio katika zoezi hili. Tunawashukuru Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed
Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu kwa kuja binafsi kutoa pole zao na
kuwafariji waliookolewa wakiwa hai kwa kuwatembelea vitandani mwao
Hospitali ya Mnazi Mmoja na pia kuwafariji wafiwa kwa kuzitembelea
maiti zilizookolewa pale uwanja wa Maisara.
Namshukuru Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa karibu nami kwani tangu ajali
ilipotokea tulikuwa tunawasiliana kwa simu na kwa mchango mkubwa
aliotoa kutoka Ofisi yake.
Ndugu Wananchi, aidha, nawashukuru Mabalozi wa nchi mbali mbali
waliokuja binafsi kutufariji na pia wale waliotupigia simu. Kwa
kipekee namshukuru Balozi Mdogo wa China hapa Zanzibar ambaye tumekuwa
naye bandarini mara tu ajali ilipotokea.
Mwisho kabisa, nawashukuru Mawaziri wote wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mawaziri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Wawakilishi kwa umoja na
mshikamano wao waliotuonyesha tangu mwanzo wa ajali mpaka sasa.
Inshallah Mwenyezi Mungu atujaalie tuendelee na mshikamano wetu huu kwa
maslahi ya wananchi wetu.
Ndugu Wananchi, nawashukuruni sana kwa kunisikiliza.
Balozi Seif Ali Iddi
MAKAMU
WA PILI WA RAIS,
ZANZIBAR.
23 Julai,
2012: