KITUO CHA WATOTO YATIMA WILAYANI MAKETE CHAIOMBA SERIKALI KUWASAMEHE KODI


Watoto yatima waliopo kituoni hapo


Mkuu wa wilaya ya Makete Josephine Matiro (kushoto) akiwa amembeba mtoto yatima anaelelewa kwenye kituo hicho

Castoel Obadia akisoma risala

 
Mkuu wa wilaya ya Makete (kushoto) akiagana na Sista Anna ambaye ni mwanzilishi wa kituo hicho

 Diwani wa kata ya Bulongwa Ericka Sanga akiagana na sister Anna

 
Moja ya jengo la kituo hicho


Na Edwin Moshi, Makete

Jamii imeshauriwa kuona umuhimu wa kutembelea watoto yatima wanaolelewa katika vituo mbalimbali kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia wao kujiona wanathaminiwa na kupendwa kama watoto wengine

Hayo yamesemwa na mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Josephine Matiro wakati alipotembelea kituo cha watoto yatima cha Bulongwa Orphans Home kilichopo kata ya Bulongwa wilayani Makete ambapo pamoja na mambo mengine ametoa msaada wa vitu mbalimbali kwa ajili ya watoto hao

Mh. Matiro amesema watoto yatima wanahitaji faraja ya hali ya juu kutoka kwa wanajamii hivyo wanapotembelewa na watu mbalimbali hujisikia faraja na kufanya maisha yao kuwa ya furaha zaidi

Amesema ameona ni vyema kuwaona watoto hao wanaolelewa kwenye kituo hicho na kutoa msaada kidogo kwa ajili ya watoto hao ili wafurahie sikukuu zilizopo mbele yao kama watoto wengine wanaoishi na wazazi ama walezi wao majumbani

“Nimeona si vyema kula sikukuu mimi kabla ya hawa watoto nimeleta hiki kidogo kwa ajili ya watoto hawa wao waanze kusherekea mapema kwa kuwa jukumu la kuwalinda watoto hawa ni letu sote, na mimi kama mkuu wa wilaya binafsi, nimeguswa na ndio maana nimekuja kuwaona” alisema Matiro

Katika hatua nyingine mkuu huyo amefurahishwa na jinsi watoto hao wanavyotunzwa na kulelewa katika maadili mema, huku akisisitiza kituo hicho kuendelea na moyo huo wa kuwalea watoto hao katika maadili mema

Akisoma risala kwa mkuu wa wilaya moja ya mtumishi wa kituo hicho aliyejitambulisha kwa jina la Castoel Obadia amesema kituo hicho kinaendeshwa kwa kutegemea misaada kutoka nje pamoja na ndani ya nchi, lakini kwa kiasi kikubwa ni kutoka kwa Sister Anna ambaye ndiye muanzilishi wa kituo hicho

Amesema mafanikio yaliyopo katika kituo hicho kuwa ni pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali ikiwemo nyumba ya kulala wageni, mashine ya kusaga na kukoboa mahindi, mashine ya kukamulia alizeti pamoja na mradi wa ng’ombe nguruwe na mbuzi ambayo kwa kiasi Fulani huwaingizia kipato inagawa hakitoshi kulingana na mahitaji ya kituo hicho

Amezitaja changamoto zinazokikumba kituo hicho kuwa ni pamoja na uhaba wa fedha za kuwalea watoto hao pamoja na wafanyakazi, uhaba wa maji,kuiomba halmashauri ya wilaya ya Makete kusamehe kutoza kodi kwenye miradi ya kituo hicho,pamoja na ukosefu wa nyumba za watumishi

Wamesema kwa kuwa mahitaji ya kituo hicho ni makubwa ukilinganisha na kipato hivyo wameona ni bora kuanzisha miradi hiyo kama njia ya kujiongezea kipato lakini wanaiomba halmashauri iwasamehe kodi ili fedha hizo zitumike kwenye kituo hicho

Mkuu wa wilaya ameahidi kuzishughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na viongozi wengine ili kituo hicho kizidi kutoa huduma ya kulelea watoto yatima

Katika ziara hiyo mkuu wa wilaya aliambatana na diwani wa kata ya Bulongwa Mh. Erica Sanga ambaye amemshukuru mkuu wa wilaya kwa moyo wake wa kutembelea kituo hicho

Kituo hicho kinapokea na kulea watoto waliofiwa na mama yao na kuendelea kuwatunza hadi pale wanapokuwa tayari kujitegemea kwa kuwa wengi hupenda kuishi hapo hata wakienda kusoma katika shule mbalimbali


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo