Wananchi wilayani Makete wametakiwa kuweka akiba
ya chakula na kuacha tabia ya kuuza mazao ya chakula pindi wanapoyavuna
Hayo yamezungumzwa na mwenyekiti wa kitongoji
cha RC “A” katani Iwawa Bw. Mapambano Mahenge wakati akizungumza na wananchi
waliohudhuria kwenye mkutano wa hadhara wa kitongoji hicho, na kuongeza kuwa
wapo wananchi wanaouza mazao yao baada ya kuvuna bila kujiwekea akiba hali
inayopelekea upungufu wa chakula miongoni mwa familia nyingi wilayani hapo
Amesema ukosefu wa chakula majumbani unaotokana
na uuzwaji wa mazao ya chakula wakati mwingine husababisha ongezeko la watoto
wa mitaani kwani watoto hulazimika kwenda mitaani kujitafutia chakula
Bw. Mahenge pia amewataka wananchi hao kutunza
mazingira ikiwa ni pamoja na kutunza vizuri mashamba yao mara baada ya kuvuna na kuepuka kuanzisha
moto kichaa ambao nao unaharibu mazingira
Akiendelea kuzungumzia suala hilo la utunzaji wa
mazingira mwenyekiti huyo pia amewataka wakazi wa Makete kutunza mazingira yao
na kuhakikisha yapo katika hali ya usafi muda wote ili kuepukana na uwezekano
wa kukumbwa na magonjwa ya milipuko yatokanayo na uchafu uliopo kwenye
mazingira wanayoishi
Na Anitha
Sanga & Obeth Ngajilo