Imeelezwa kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili
wauguzi wilayani Makete zikitatuliwa kwa wakati itasaidia kuboresha huduma
mbalimbali zinazotolewa na wahudumu hao wa afya wilayani hapo
Hayo yamebainika wakati risala ya wauguzi kwa mgeni rasmi
wakati wa maadhimisho ya siku ya wauguzi duniani yaliyofanyika kiwilaya katika
hospitali ya wilaya ya Makete
Wauguzi hao wamesema kutokupewa mishahara kwa wakati hasa
kwa watumishi wapya hupelekea baadhi ya waaajiriwa hao wapya kutoroka mahala pa
kazi, na pia watumishi kutotatuliwa matatizo yao kwa wakati, ikiwemo
kutopandishwa vyeo kwa wakati hali inayopelekea kazi kutofanyika kwa moyo
Akihutubia katika maadhimisho hayo mgeni rasmi ambaye pia
ni Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete Bi Imelda Ishuza amekiri
kuwepo kwa changamoto hizo na kusema kuwa baadhi ya changamoto zimeshaanza
kufanyiwa kazi, ikiwemo ya kulipa mishahara kwa wakati pamoja na watumishi hao
kupandishwa vyeo
Amesema Mei 21 mwaka huu kutakuwa na kikao na bodi ya
ajira kwa lengo la kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo la watumishi
kupandishwa vyeo, hivyo kuuagiza uongozi wa hospitali ya wilaya kukaa na
kupeleka majina ya watumishi wanaotakiwa kupandishwa vyeo
Kuhusu suala la mishahara kuchelewa Mkurugenzi huyo
amesema utaratibu wa sasa wa kutuma taarifa za watumishi wizarani kwa kutumia
mtandao, utasaidia kuondoa kero hizo za watumishi
Katika maadhimisho hayo kila mshiriki aliwasha mshumaa
kama ishara ya upendo na kumkumbuka muuguzi wa kwanza marehemu Florence
Nightngale, pamoja na mgeni rasmi kutembelea wodi zote za hospitali ya wilaya
ya Makete kuwapa pole wagonjwa waliolazwa katika hospitali hiyo
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni KUBORESHA
HUDUMA KWA VITENDO