MAKETE 12.04.2011
Mawasiliano ya barabara itokayo Makete hadi Njombe yamekatika usiku wa kuamkia leo baada ya maporomoko ya udongo yanayodhaniwa kuwa mfano wa volcano kufukia barabara hiyo eneo la kilanzi kata ya Lupalilo wilayani Makete na kupelekea mawasiliano hayo kukatika kabisa
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia wamesema tukio hilo limetokea kati ya saa mbili na saa tatu jana usiku na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo
Udongo huo mbali ya kufunga barabara hiyo pia umefunika milingoti ya miti mikubwa iliyokuwa katika eneo hilo na udongo huo kusambaa eneo kubwa kama vile ulikuwa ukitawanywa na katapila la kutengeneza barabara
Akizungumza katika eneo la tukio leo asubuhi, mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Zainab Ahmad Kwikwega amewataka wananchi kuwa na moyo wa subira kwani serikali ipo pamoja nao katika wakati huu mgumu wa kukatika kwa mawasiliano hayo
Aidha amesema jitihada zilizochukuliwa na ofisi yake mpaka sasa ni kutengeneza njia ya dharura ambayo ni kwa ajili ya watu waendao kwa miguu peke yake ambayo itatumika mpaka hapo ufumbuzi utakapopatikana kwani taarifa hizo zimeshafika hadi ngazi ya taifa
Abiria watokao makete-Njombe wanaishia eneo la tukio na kuvuka ng’ambo ya pili ambako wanakuta magari mengine na wanaendelea na safari zao licha ya kupata usumbufu mdogo wa kuvukia ng’ambo ya pili kupitia njia hiyo ya dharura
P.T.O
Katika kuonesha hali ya kuguswa na janga hilo Kaimu mkuu wa mkoa wa Iringa ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Morogoro Kanali Mstaafu Issa Salehe Machibya amefika katika eneo la tukio na kujionea hali ilivyo huku akisomewa taarifa fupi ya tukio hilo na Mkuu wa wilaya ya Makete Mh. Zainab Kwikwega
Akizungumza na wananchi mara baada ya kupokea taarifa hiyo, Kaimu mkuu huyo wa mkoa amesema kutokea kwa maporomoko hayo ni mpango wa MUNGU hivyo wananchi wawe na subira kwani serikali italishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo
Amesema ofisi yake imeshazitoa taarifa hizo ngazi ya taifa na wataalamu watafika mara moja ili kufanya uchunguzi wa kina wa maporomoko hayo ambayo bado yanaumiza vichwa vya watu wengi
Mbali na mkuu wa mkoa pia kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Iringa nayo imefika ili kujionea hali ilivyo
Kwa mantiki hiyo watumiaji wa barabara ya makete njombe kwa sasa mnataarifiwa kutotumia barabara hiyo na badala yake zitumike barabara mbadala ambayo ni ya Makete – Bulongwa hadi Mbeya au Makete hadi Mfumbi na kutokea Chimala
Tukio hili limegusa hisia za watu wengi kwani inaaminika kuwa miaka ya 90 maporomoko kama hayo yaliwahi kutokea maeneo ya Luwumbu.
TAARIFA ZAIDI UTAJULISHWA KWA KADRI NINAVYOZIDI KUZIPATA!