Mwanamume mmoja anadaiwa kumkata mwenzake sehemu za siri kutokana na deni la Sh50.
Kisa hicho kilizua rabsha katika mji wa Kutus, Kaunti ya Kirinyaga, Ijumaa huku wenyeji waliokuwa na hasira wakitaka haki itendeke.
Inasemekana mwathiriwa alipigana na mchinjaji wa eneo hilo siku ya Alhamisi usiku.
Mwathiriwa kwa sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya. Wakati wa ugomvi huo, mashahidi wanadai kuwa mfanyabiashara huyo alimburuta mwathiriwa hadi kwenye duka lake na kumkatakata.
Mwanamume aliyejeruhiwa, Muthii, alijikwaa hadi mahali pa kazi akivuja damu nyingi kabla ya kuzimia, kulingana na mkazi wa eneo hilo.
Mara moja alipelekwa kwenye zahanati ya karibu kwa ajili ya huduma ya kwanza, kwa ushauri wa mwajiri wake.
Kwa sasa anapigania maisha yake katika Hospitali ya Rufaa ya Kerugoya baada ya kuelekezwa huko.
Wakiwa wamekerwa na tukio hilo la kustaajabisha, wenyeji hao walitishia kuchukua hatua mikononi mwao iwapo mshukiwa hatawekwa chini ya ulinzi.
Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani kutawanya umati huo wenye hasira kutokana na mvutano huo uliokuwa ukiongezeka.
Chanzo:Radio Jambo