POLISI
Jijini Arusha imewaachia kwa dhamana watu wanaotuhumiwa kurusha bomu
kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, lililopo Jijini
hapa. Aidha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
alisema, wanaendelea kuwahoji zaidi watu hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo, Kamanda Sabas amesema, wameamua kuwaachia
kwa sababu sheria haiwaruhusu kuendelea kuwashikilia muda mrefu.
“Na lengo letu hasa katika hili tukio hatutaki kumwonea mtu yeyote, ndio sababu tunafanya uchunguzi wa kina,” alisema Sabas.
Alisema
watuhumiwa hao ni lazima waripoti polisi, pale wanapohitajika. Alisema
hadi sasa hakuna mtu mwingine aliyekamatwa au kufikishwa mahakamani
zaidi ya Victor Ambros aliyefikishwa mahakamani.
Ambros
alifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuua na kukusudia kuua
huku wengine wanne, raia wa nje ya nchi wakiachiwa huru.
Awali
watuhumiwa waliokuwa wakiendelea kushikiliwa kwa uchunguzi zaidi ni
Jassini Mbarak (29) mkazi wa Bondeni Arusha, Joseph Lomayani (18) dereva
wa pikipiki mkazi wa Kwa Mrombo Arusha, Batholomeo Silayo (23)
mfanyabiashara mkazi wa Olasiti na Mohamed Suleiman Said (38) mkazi wa
Ilala Jijini Dar es Salaam.
Raia
wa Falme za Kiarabu ambao wote walioachiwa huru, ni Abdulaziz Mubarak
(30) (Saudi Arabia), Foud Saleem Ahmed (28), Said Mohsen na Said
Abdallah Said (28).
Wote
wanaishi nchini humo. Bomu hilo lililorushwa Mei 5, mwaka huu, saa 4.30
asubuhi, lilisababisha vifo vya watu watatu na majeruhi wapatao 60.
Majeruhi
hao walipatiwa matibabu katika Hospitali za Mount Meru na St. Elizabeth
na baadhi yao walihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam
kwa matibabu zaidi.
Katika
ibada hiyo ya uzinduzi wa Parokia mpya ya Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
mgeni rasmi alikuwa Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco
Padilla, akisaidiana na Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha, Joseph Lebulu.
CHANZO HABARI LEO
