Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Jokate Mwegelo amewasihi Wanawake kutowatupa Watoto na kuwaomba wawe wavumilivu wanapokumbana na stress za kubeba mimba na malezi, hii ni baada ya Mzazi mmoja ambaye hajafahamika kumtupa Mtoto wake katika Kijiji cha Kwenangu Wilayani Korogwe Mei 16, 2023.
Jokate amesema baada ya kuokotwa mtoto huyo alipelekwa Kituo cha Afya Mkumbara na kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya Magunga ambako aliendelea kupata matibabu na sasa afya yake imeimarika na leo anapelekwa kituo cha kulelea Watoto yatima Ilente wilayani Lushoto.
Jokate amesema; “Mtoto amepewa jina la Brigita Ustawi Korogwe, jina la DMO Korogwe Vijijini, wakati Wanawake wengi wakiwa wanatafuta Watoto wapo ambao Mungu anawabariki Watoto ila wanawatupa.
"Nawasihi nafahamu kuna stress nyingi zinaambatana na kubeba mimba na malezi lakini baraka aliyotupa Mungu ya kuleta kiumbe chake duniani naona ni thawabu na zawadi kubwa mno kuliko changamoto tunazopitia Kama wakina mama.”
“Tukaze mwendo Mungu mwenyewe huleta baraka zake kupitia hawa Malaika na vizazi vyetu, kwa atakayeguswa kuchangia mahitaji ya Mtoto tafadhali wasiliana na Afisa Ustawi wetu wa Halmashauri ya Korogwe Vijijini kupitia namba hii +255 712 275 585.”