Adaiwa Kumuua Babake, Aupika na Kuula Mwili Wake

 


Mwanaume kutoka kijiji cha Giankaja, kaunti ya Tharaka Nithi NCHINI Kenya alitiwa mbaroni baada ya kudaiwa kumuua baba yake na kupika sehemu za mwili wake.


Mwanamume huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi kaunti ya Tharaka Nithi.


Polisi walithibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha wakisema mwathiriwa ambaye ni mzee mwenye umri wa miaka 70, aliripotiwa kutoweka kwa siku tatu. Msako ulifanyika katika kijiji kizima na wakazi wa eneo hilo katika juhudi za kumtafuta mzee huyo.


Baada ya saa kadhaa za msakao, upekuzi wao uliwaelekeza kwenye mtaro wenye kina kirefu ambapo waliupata mwili wa marehemu ambao tayari ulikuwa umeshaanza kuoza. Marehemu alikuwa amekatwa kichwa na sehemu za mwili wake kukatwa na miguu yake ikiwa kando ya mwili wake. 


Walikimbia haraka kwa chifu wa eneo hilo ili kumjulisha kuwa wamempata mtu aliyepotea. Hata hivyo, waliporejea kwenye mtaro, mwili huo haukuonekana.


Wakiwa wamechanganyikiwa na jinsi mambo yalivyobadilika, wenyeji hao katika udadisi wao pamoja na polisi na chifu walitafuta ndani zaidi ya mtaro. Walizunguka kwenye mtaro wa kina kirefu uliowaelekeza kwenye nyumba ambayo polisi wanasema huenda ilikuwa ya mshukiwa. Walipofika katika nyumba hiyo, walishangaa kupata chungu cha kupikia kimejaa nyama na mboga. 


Katika eneo la tukio, kulikuwa na fuvu la kichwa cha binadamu na nguo zilizojaa damu pamoja na viatu vya marehemu. Polisi walimhoji mshukiwa huyo kuhusu aliko baba yake lakini alibaini kuwa pia alikuwa hafahamu kwa kuwa anaendelea kumtafuta.


Sehemu nyingine za mwili zilizopotea ambazo ziligunduliwa kwanza na wenyeji zilipatikana zikiwa zimetupwa kwenye gunia na kufunikwa kwa mawe ndani ya Mto Nithi. 


Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye alidai kuwa mshukiwa huyo alianza kuchimba mtaro huo mwaka 2017, alieleza kuwa mshukiwa na mwathiriwa wake walizozana kuhusu hali ya mtaro huo kabla ya kupotea. "Wawili hao walizozana baada ya mwanamume huyo kumzuia babake kukata nyasi za Napier kuzunguka mtaro," Johnson Mutembei mkazi aliambia jarida moja la eneo hilo.


Kwa sasa mshukiwa yuko rumande akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.


Chanzo: TUKO.co.ke 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo