Watu wengi wamekuwa wakiamini kuwa serikali haiamini uchawi na hakuna sheria inayombana mtu katika masuala hayo, lakini ukweli ni kwamba kifungu cha sheria ya uchawi kipo na watu hupewa hukumu pale wanapobainika kuhusika na masuala hayo.
Deogratius Massawe ni Mkuu wa Polisi wilaya ya Ludewa Mkoani Njombe amefika katika kijiji cha Kiyogo kilichopo katika kata ya Masasi na kutoa elimu hiyo katika mkutano wa hadhara baada ya hivi karibuni kijijini hapo kutokea tukio la baba mmoja aliyefahamika kwa jina la Lucas Mahundi kupigwa na kujeruhiwa na watoto wake wakimtuhumu kumuua mama yao kichawi kwa kutumia mamba.
Kwa upande wa Lucas Mahundi ambaye ndiye aliyejeruhiwa na watoto wake hao amesema kujeruhiwa kwake hakuhusiani na tuhuma za uchawi lakini wananchi wenzake walipinga kauli hiyo na kumtaka kuwa muwazi huku wengine wakieleza namna ambavyo wachawi hutumia mamba kuondoa uhai wao.