Mhubiri Ezekiel Odero wa kanisa la New Life Prayer Centre katika kaunti ya Kilifi alikamatwa mnamo Alhamisi - Aprili 27, 2023 akihusishwa na injili ya itikadi kali.
Kwa mujibu wa People Daily, makachero wanaochunguza vifo vya waumini eneo la Shakahola ambako zaidi ya miili 100 imefukuliwa kufikia sasa wanadai kuwa Ezekiel huenda alishirikiana kwa ukaribu na Paul MacKenzie kuficha vifo vilivyotokea katika kanisa lake la Mavueni.
"Uchunguzi wa mwanzo umefichua kuwa Pasta Ezekiel anadaiwa kusafirisha miili ya wale waliofariki katika kanisa lake hadi Shakahola kwa usaidizi wa Mackenzie," polisi wamesema kupitia kwa taarifa.
Inaarifiwa kwanza miili hiyo kwanza ilipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Milele lakini mhubiri huyo akatofautiana na hifadhi hiyo kwa malipo.
Ezekiel alituhimiwa na makafani hayo ya Milele kwa kukosa kulipa bili ya mochari kwa waumini waliofariki katika kanisa lake. Kwa mujibu wa polisi, baada ya kutofautiana na makafani hayo, Ezekiel aliichukua miili hiyo, kuiweka katika lori kisha kuisafirisha hadi Shakahola na kuizika kisiri.
"Miili hiyo inaaminika kutolewa katika Hifadhi ya Maiti ya Milele baada ya pasta kutofautiana na uongozi wa makafani hayo," taarifa ya polisi imeongeza.
Chanzo: TUKO.co.ke
