Watu saba kutoka kaya nne tofauti wamefariki baada ya kula nyama ya samaki aina ya kasa anayesadikiwa kuwa na sumu, Kaimu RPC Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Canute Msacky amesema tukio hilo limetokea March 12,2023 katika Kijiji cha Bweni na Kijiji cha Kanga, Kara ya Kanga, Wilaya ya Mafia.
Majina ya waliofariki katika tukio hilo ni Abdallah Hatibu Nyikombo (4), Makame Hatibu Nyikombo (9), Mohamedi Juma Makame (Miezi 7), Ally Selemani (Miezi 8), Salima Omary Mjohi (28), Minza Juma Hatibu (Miezi 10) na Ramadhani Karimu (Miezi 8).
Watu hao walifariki majira tofauti tofauti na miili yao imefanyiwa uchunguzi wa kitabibu katika Hospitali ya Wilaya Mafia na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi “Chanzo cha tukio hilo bado kinaendelea kuchunguzwa, Watuhumiwa watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya Mafia kwa mahojiano zaidi, katika hatua hiyo Watuhumiwa hao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mafia baada ya kuzidiwa wakiwa chini ya uangalizi wa Jeshi la Polisi, kwani nao walikula nyama ya samaki huyo”
“Polisi inatoa wito kwa Wavuvi Wilaya ya Mafia kuacha tabia ya kuvua samaki aina ya kasa ambao ni nyara za Serikali, bali wafuate taratibu na sheria za uvuvi wa samaki hao, Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kali kwa Wavuvi wasiofuata taratibu na sheria za Nchi”