Muhubiri wa Jijini Mwanza, Diana Bundala maarufu ‘Mfalme Zumaridi’ ambaye hivi karibuni aliachiwa huru baada ya kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani, amesema katika maisha yake amekuwa na mfululizo wa matukio ya kutokewa na Mungu kwa njia mbalimbali lakini kwa mara ya kwanza alitokewa na Mungu kwa njia ya jua akiwa darasa la tatu.
Kwenye mahojiano yake na Millard Ayo, Diana amesema jua hilo lilimtokea wakati akiwa amelala na kisha kueleza kuwa Mungu alitaka kumtumia yeye na kutoa ubatizo wa roho kwa Wanadamu na kuwaokoa na dhambi za dunia.
“Nikiwa darasa la tatu nilitokewa na Mungu katika umbo la jua. Nikiwa nimelala na mama usiku lilikuja jua jeupe likamulika ndani pote pakawa na mwanga mweupe sana.
“Lile jua likaanza kusema na mimi, Mimi ni Mungu, Mimi ni Mungu, Mimi ni Mungu, sina mwili, sina mwili, sina mwili, mimi ni roho, mimi ni roho, mimi ni roho mpaka mara tatu. Nimekuja kusema na wewe.
“Lile jua lilikuwa likichezacheza huku sauti ikitoka, nilishtuka lakini baadaye nikatulia, nikaanza kusikiliza… Kama nilivyokaa ndani ya Yesu Kristo kama roho kwa ajili ya kuokoa wanadamu, na sasa mwili wa Yesu Kristo haupo tena Duniani na miili ya Mitume haipo tena Duniani.
“Ninahitaji nikutumie mimi Mungu, ninahitaji nikatoe ubatizo war oho kwa wanadamu. Kwa sababu dhambi zote za wanadamu zipo katika roho na sio mwili. Ndiyo maana mimi Mungu ninahukumu roho na si mwili.
“Mwanadamu anatenda dhambi katika roho kwa kufukiri kwanza ndipo anatenda na hatendi katika mwili… likaongea lile jua kisha likaaga Kwa Heri, likaja kwenye mwili wangu likapotelea humo, nikashtuka nikaanza kutetemeka,” amesema Zumaridi.