Kituo Jumuishi Huduma za Kimahakama, Mirathi na Ndoa, Temeke kimeivunja rasmi ndoa kati ya wanasiasa machachari David Kafulila na Jesca Kishoa kupitia shauri la ndoa No 217 ya 2022.
Ndoa hiyo iliyofungwa Aprili 22, 2014 ilivunjwa rasmi Februari 20, 2023 baada ya wanandoa hao kutengana tangu mwaka 2019 kabla Mahakama ione ndoa hiyo imevunjika kiasi cha kutorekebishika.
Wakati hati ya madai ikionyesha kiini cha mgogoro huo ni ugomvi na utengano, Mahakama imevunja ndoa baina ya wawili hao huku ikitoa amri kwa mama kubaki na watoto na kila mzazi kuwa na wajibu wa kuchangia gharama za matunzo kwa asilimia 50.
“Maombi ya Jesca Kishoa akiitaka Mahakama ione ndoa kati yake na David Kafulila imevunjika kiasi cha kutorekebishika na kuomba amri ya Mahakama kuvunja ndoa hiyo, mjibu maombi aliwasilisha majibu yake na hakuwa na pingamizi juu ya maombi yaliyopo mahakamani.
“Eden Kilatu na rashid Hussein, mawakili wasomi wamemwakilisha mleta maombi na mjibu maombi mtawalia. Kilatu ameiomba Mahakama itoe hukumu kwa kuzingatia shauri la Joseph Warioba Butiku vs Perucy Muganda Butiku (1987) TLR 1,” alieleza nakala ya hukumu iliyotolewa na Hakimu Mwandamizi Swai.S.O.
Hakimu Swai ameeleza kwa upande wake hana mashaka kuwa ndoa ya wadaawa imevunjika kiasi cha kutorekebishika chini ya kifungu 107 (2) (f) cha sheria ya ndoa.
“Kwa msingi huo amri ya kuivunja ndoa na talaka inatolewa. Sambamba na hilo, watoto wataishi chini ya uangalizi wa mama yao. Mjibu maombi atakuwa na haki ya kuwaona na kuwa na watoto wake mwishoni mwa juma na vipindi vya likizo za masomo,” ameeleza Jaji Swai.
Katika hukumu hiyo ameeleza kuwa chini ya kifungu 129 cha Sheria ya Ndoa, mjibu maombi anawajibika kutoa matunzo ya watoto kikamilifu.
“Ada za shule zitaendelea kulipwa kwa uwiano linganifu (asilimia 50) kwa kila mzazi katika shule watakazokubaliana pamoja. Hayo ndiyo maamuzi ya Mahakama. Kutokana na asili ya shauri hili hakuna amri ya gharama inatolewa. Imeamuliwa na kuagizwa hivyo,” imeeleza Hakimu Swai.
Chanzo:Mwananchidigital