Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi nchini, Anna Makinda amesema maadili ya Kitanzania yanazidi kushuka kila kukicha kutokana na mpangilio wa nyumba za watu kulala chumba kimoja na watoto wao.
Makinda ameyasema hayo Machi 10, 2023 mjini Babati mkoani Manyara ambako alifanya ukaguzi kwa wataalamu wanaofanya uchambuzi wa takwimu za makazi.
Amesema watu wanazaliana bila kujua utaratibu wa mahali pa kuishi kuwa linalochangia kushuka kwa maadili kutokana na ujenzi wa nyumba duni. Licha ya kushuka kwa maadili, pia kunachangia mafuriko ya maji kutokana na msongamano wa makazi hayo ya watu.
"Watu wanazaliana sana bila hata kujua wanaweza kuishi wapi. hili nalo ni tatizo la nchi na linachangia maadili kushuka kila kukicha na kusababisha ongezeko la watu wasio na makazi," amesisitiza.
Amesema ongezeko hilo linachangia pia mafuriko kwenye makazi ya watu na kudai kuna haja ya kutazamwa upya namna bora kukabiliana na tatizo hilo.