Mwanamume mwenye umri wa makamo anadaiwa kujitoa uhai katika boma la wakwe zake katika kijiji cha Kolondo, kaunti ndogo ya Rachuonyo Mashariki, kaunti ya Homa Bay nchini Kenya, baada ya mazungumzo ya kurudiana na mke wake kugonga mwamba.
Mwanamume huyo kutoka kaunti jirani ya Kisii alikuwa amewatembelea wakwe zake katika juhudi za kupatanishwa na mke wake ambaye walitengana hivi majuzi kufuatia ugomvi wa kinyumbani. Lakini mazungumzo hayo yanasemekana kugonga mwamba huku mwanamume huyo akiondoka nyumbani kwa wakwe zake akiwa na hasira.
Chifu wa eneo la Atela Perez Okoth alithibitisha kisa hicho, akisema mwili wa mwanamume huyo ulipatikana ukining'inia kwenye mti ulioko karibu na nyumba ya mama mkwe wake Jumapili, Machi 12 asubuhi.
"Mwanamume huyo anasemekana kutofautiana na mkewe ambaye alirudi nyumbani kwao. Kisha alimfuata mkewe ambaye alikuwa amerejea nyumbani kwao ili kusuluhisha tofauti hizo ili waweze kuungana tena kama familia, hata hivyo, mazungumzo yalionekana kugonga mwamba alinyimwa mkewe.
Sio kisa cha kwanza Kulingana na wanakijiji, tukio hilo la Jumamosi ni la pili kuripotiwa katika boma hilo. Inadaiwa kuwa mwanamume mwingine pia alijitoa uhai nyumbani humo katika hali sawia na hiyo.
Chifu wa eneo hilo hata hivyo alitoa wito kwa familia kutafuta njia mwafaka za kutatua masuala kinyumbani ili kuepukana na matukio kama hayo. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Rachuonyo kusubiri uchunguzi wa maiti na polisi.
Chanzo: TUKO.co.ke