Na Farida Mangube, Morogoro
MTU ambaye jina lake halijafahamika amefariki Dunia na mwili wake kukutwa ukielea kwenye dimbwi la maji katika Mtaa wa Fungafunga kwenye Kata ya Kichangani Manispaa ya Morogoro.
Kwa mujibu wa wananchi wa maeneo hayo wanaeleza kwamba tukio la kukutwa mtu amekufa ni la tatu kuripotiwa kutokea katika Kata hiyo kwa kipindi cha hivi karibuni.
Akizungumza na Waandishi Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Morogoro Emmanuel Ochieng amesema walipokea taarifa toka kwa raia wema kueleza uwepo wa tukio hilo na baada ya kuopoa mwili wamekabidhi katika mamlaka nyingine Hospitali ya Rufaa mkoa wa Morogoro ili kuendelea na uchunguzi zaidi kwakua bado haijafahamika chanzo halisi cha kifo chake.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kichangani Girbert Barnabas ameviomba vyombo vya usalama kuchunguza kwa makini chanzo cha kifo pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika Kata hiyo.
" Ingawa bado haijathibitika sababu hasa ya kifo, ipo haja ya vyombo vya usalama kuja na majibu halisi kubaini chanzo cha matukio hayo yanayoripotiwa mara kwa mara katima kata yangu," amesema.
Imeelezwa kwamba eneo ambalo tukio limefanyika kunafanyika shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufyatuaji wa matofali, na sio mara ya kwanza kuripotiwa matukio ya aina hiyo. Wenyeji wanasema baadhi ya watu wamegeuza kuwa sehemu ya kificho kwani hufanya uhalifu maeneo mengine.
Kwa mujibu mashuhuda wameeleza historia inaonesha miaka ya nyuma eneo hilo kulikua na makazi ya watu na Serikali ikalazimika kuwahamisha kwa sababu eneo hilo hujaa maji inapofika msimu wa mvua na sasa linatumiwa na baadhi ya watu kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo na kufyatua matofali, shughuli ambazo pia hufanyika kinyume kwakua kulisha tolewa makatazo.