Familia ya Marehemu Swalehe Mshale (74) wa Mbagala Majimatitu A Wilaya ya Temeke Jijini Dar es Salaam, imeiomba Serikali kuwafutia deni la milioni 10 wanalodaiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambalo limefanya wasiruhusiwe kuchukua mwili wa mpendwa wao mochwari.
Mzee Swalehe alifariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Februari 10 2023 wakati akipatiwa matibabu kutokana na utumbo wake kutoboka na hadi sasa ni siku ya tano wameshindwa kuuchukua mwili wake kwa ajili ya mazishi kutokana na deni wanalodaiwa la milioni Kumi ambapo wanasema wameambiwa watoe asilimia 75 ya deni ndipo wapewe mwili wa Mpendwa wao.
"Tulikuwa na Mgonjwa Muhimbili Hospitali alilazwa Kibasila wodi namba 11 akahamishiwa Mwaisela ICU namba 2 kwa ajili ya matibabu zaidi kwa sababu hali yake haikuwa nzuri hadi Februari 10 akafariki ambapo nikaambiwa nikafunge bili, nikakuta nadaiwa milioni kumi na laki sita lakini kutokana na hali yangu ngumu ya kiuchumi nikaambiwa nifate process ili tupate msamahama ambapo tuliandikiwa barua na Serikali ya Mtaa tukaenda hadi Muhimbili Ustawi wa Jamii ndipo tukaambiwa tulipe asilimia 75 ya pesa sawa na milioni nane".
"Uwezo wetu ni mdogo sana, kama Serikali inaweza kutupa mwili wetu tutashukuru sana lakini kama haiwezekani basi itabidi sisi tuache tuangalie taratibu nyingine maana hadi sasa tumefanikiwa kukusanya shilingi milioni moja tu" amesema Stumai Mshale, Ndugu wa Marehemu.
Tunaendelea kuutafuta Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili ili kusikia kutoka upande wao.
Chanzo:Ayo TV