Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano na wale walio katika taasisi za elimu wawe wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro pia amesema amepokea maelekezo kutoka kwa Rais Samia kuwa watu wazima wawekewe mikakati ili ifikapo mwaka 2030 kila mwananchi awe na cheti cha kuzaliwa.
Dk Ndumbaro alisema ni lazima usajili ufungamanishwe na taasisi za elimu ili wakati wa usajili wa kujiunga na elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu wote wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa wapate fursa kupitia kambi maalumu ya usajili.
Alisema hayo jijini Dodoma wakati akizindua Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA).
Dk Ndumbaro alisema usajili wa matukio muhimu ya binadamu ni nyenzo muhimu ya kuipatia serikali takwimu katika kupanga mipango ya maendeleo na usalama wa nchi.
“Natoa maelekezo kwa RITA kuanzia sasa usajili ufanyike kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zote za serikali na watu binafsi, kwenye taasisi za elimu, kuanzia shule za awali, msingi, sekondari na vyuo mbalimbali lengo likiwa kuwafikia wananchi wengi zaidi,” alisema.
Dk Ndumbaro aliiagiza bodi hiyo ya ushauri iishauri wizara kuhusu mambo ya kisera na utekelezaji wa majukumu ya RITA ili kuisaidia serikali katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.