Mkuu wa Wilaya ya Iringa Veronica Kessy amewaomba radhi wazee wa Manispaa ya Iringa kufuatia uvamizi wa baadhi ya watu ambao wanadhaniwa kuwa ni wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama machinga kwa kitendo cha kuvamia eneo la makaburi ya Samora na kuanza kusafisha wakidai wanataka eneo hilo litumike katika shughuli zao.
Kessy amelaani vikali kitendo hicho ambacho kimefanywa na watu hao kwa mihemuko yao binafsi na kusema kuwa kitendo hicho sio sahihi na ni uvinjifu wa heshima kwa ndugu zetu ambao wamepumzishwa katika eneo hilo.
Amesema Manispaa ilipewa agizo la kuhakikisha wanatafuta eneo ambalo ni sahihi kwa machinga na tayari limekamilika ambapo agizo hilo lilitakiwa kukamilika mnamo Februari 24 mwaka huu.
Amesema tayari Manispaa imekamilisha eneo la uendeshaji wa biashara hizo katika eneo la mrandege lilopo Manispaa ya Iringa na agizo limetolewa kwa machinga kuhamia katika eneo hilo Machi Mosi mwaka huu.