Baba wa Watoto 102 Asema Ameshindwa Kuwalisha "Nimeelemewa jamani"

Kwa miaka mingi, kuwa na watoto 102 ilikuwa kama mzaha kwa Musa Hasahya Kasera mwenye umri wa miaka 68 kutoka kijiji cha Bugisa, wilaya ya Butaleja, mashariki mwa Uganda.


Alianza kuwa kivutio cha watalii baada ya habari kuenea kwamba ana wake 12, wajukuu 578, na kwamba hakumbuki majina ya wengi wa watoto wake. Sasa mwanamume huyo amejikuta katika taabu kwani ameshindwa kuwalisha wanawe na kuwajukumikia kwa sababu ya uidadi yao. 


Kasera alifichua kuwa kwa sasa hana kazi jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa kwake, Daily Nation iliripoti.


Hiyo inaeleza kwa nini hivi majuzi aliwataka wake zake wote wapange uzazi ili kukomesha kujifungua watoto zaidi kuepukana na changamoto za maisha. “Sitarajii kupata watoto zaidi kwa sababu nimejifunza kutokana na kitendo changu cha kutowajibika cha kuzaa watoto wengi ambao nimeshindwa kuwalea,” alisema mwanakijiji huyo. 


Aliongeza kuwa afya yake inadhoofika na anahofia kwamba ekari mbili za ardhi anazomiliki hazitoshi kwa familia yake kubwa. Kasera pia alifichua kuwa wake zake wawili waliondoka kwa sababu hawakuweza kuendelea kukaa katika ndoa bila mambo ya msingi kama vile chakula na mavazi. 


"Mwanzoni ilikuwa mzaha... lakini sasa hii ina matatizo yake," alilalamika. Siku zile akiwa mchanga ambapo Kasera alikuwa na biashara iliyonawiri ya kuuza ng’ombe na duka la nyama, wazazi walimpa binti zao awaoe.


Familia ilipozidi kuwa kubwa mzee huyo alishindwa kukumbuka majina ya wanawe wote na hivyo basi anakumbuka tu lile la kifungua mimba na kitinda mimba wake. 


Watoto 102 wa Kasera ni kati ya umri wa miaka 10 hadi 50, wakati mke mdogo ana umri wa takriban miaka 35, wengi wao hawajasoma. 


Mbali na watoto hao, mzee huyo hulazimika kushauriana na mmoja wa wanawe aitwaye Shaban Magino, mwalimu wa shule ya msingi mwenye umri wa miaka 30, ili kumkumbusha majina ya wake zake.


Chanzo: TUKO.co.ke


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo