Mkazi wa mtaa wa Kilimahewa, mji mdogo wa Katoro wilayani Geita, Elinata Elias (27) ameuawa kwa kushambuliwa kwa mapanga katika tukio lililotekelezwa na mwanaye wa kambo, Jackson Msafiri (25).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Safia Jongo amethibitisha leo kutokea kwa mauaji hayo na kueleza tukio lilitokea Febaruari 16, 2023 majira ya saa mbili na nusu usiku.
ACP Jongo amesema mtuhimiwa alitekeleza mauaji hayo akiwa ameambatana na rafiki yake, na muda mchache baada ya tukio wahusika walishambuliwa na wananchi wenye hasira kali hadi kuuawa.
Amesema uchunguzi wa awali umebainisha chanzo cha tukio ni kijana huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa akimtuhumu mama wa kambo kutumia mali za baba yake, huku yeye akiwa hanufaiki.
Ameeleza, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kuwabaini wahusika wengine waliojichukulia sheria mkononi kwa kuwashambulia hadi kuwaua watuhumiwa wa mauaji ya mama huyo.