New York imekuwa jimbo la sita nchini Marekani kuhalalisha mtu kugeuza mwili wake kuwa udongo baada ya kifo chake, hatua iliyoonekana kama mbadala wa mazingira rafiki kwa kuzika au kuchoma maiti.
Utaratibu huo pia unajulikana kama upunguzaji wa kikaboni asilia ambapo mwili huwekwa kwenye kontena maalum pamoja na vifaa vilivyochaguliwa kama vile mbao, nyasi au majani na kuruhusiwa kuoza kwa muda wa wiki kadhaa.
Baada ya takribani mwezi mmoja na udongo ukishaondolewa vijidudu vyote vya kuambukiza kwa njia ya joto, udongo hutolewa kwa wapendwa wao na kutumika kwa kupanda miti, mboga mboga au maua.
Kwa mujibu wa BBC watetezi wa uwekaji mboji (mbolea) wa binadamu wanasema kuwa sio tu chaguo rafiki zaidi wa mazingira, lakini pia ni chaguo bora zaidi hasa katika miji ambayo nafasi ya makaburi ni ndogo.
Hata hivyo, Maaskofu wa Kikatoliki huko New York walipinga hatua hiyo kwa sababu waliamini kwamba mabaki ya binadamu hayafai kutendewa kama takataka za nyumbani.