Kijiji kimoja katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania wameshangazwa na tukio la kijana aliyesemekana kufariki na kuzikwa mnamo Aprili mwaka 2022 kurudi nyumbani kwao akiwa mzima Desemba 28.
Kulingana na taarifa zilizopeperushwa na vyombo mbalimbali vya habari katika taifa hilo jirani, Henry James mwenye umri wa miaka 28 (pichani juu) alifariki dunia Aprili kutokana na ajali ya barabarani na hafla ya mazishi kufanyika nyumbani kwao.
Cha kushangaza ni kwamba baada ya miezi kadhaa, mnamo Desemba 28, 2022 alirudi nyumbani kwa mshangao wa kila mtu, huku akisema kuwa walipokuwa wanauzika mwili uliodhaniwa kuwa wake alikuwa pembeni kwenye mti akifuatilia tukio zima.
“Mlipokuwa mnazika nilikuwa nimesimama pembeni kwenye mti.”
Schola Bukuru, mamake kijana huyo aliyekuwa amejawa na wasiwasi mkubwa kwenye panda la uso alisema kuwa alidhibitisha ukweli huyo kijana ni mwanawe ambaye waizika Aprili 2022 na hakuwa anaelewa ni kwa jinsi gani alipata kurejea nyumbani tena akiwa hai.
“Huyu ni Mtoto wangu kabisa na aliyefariki alikuwa ni huyu ila nashangaa kurudi kwake wakati sisi tulimzika hii naona ni miujiza ya Mungu, kwasababu tulipokuwa tunamzika nililia sana nikimwambia Mungu naomba unisaidie sababu nilipata misiba ya kufatana ya Watoto wangu wawili hadi nikahisi vibaya,” Bukuru alinukuliwa na Ayo TV.
Tukio hilo lisilo la kawaida lilifikia mpaka serikali ambapo kamanda wa polisi wa mkoa wa Kigoma, magharibi wa Tanzania alidhibitisha na kusema kuwa dola imelivalia njuga suala husika na ikiwezekana wataruhusu kufukuliwa kwa mwili uliozikwa Aprili ukidhaniwa kuwa wa kijana huyo ili kufanyiwa vipimo vya kisayansi, DNA.