Rais Samia atoa angalizo

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema viongozi wote waliobeba dhamana ya kulitumikia taifa, watambue kwamba Watanzania wana matumaini makubwa kwao, hivyo wazingatie uadilifu, kufuata misingi ya haki na sheria.


Vilevile, Mkuu wa Nchi amesema mwaka 2023 unapswa kuwa kielelezo kuliko miaka iliyopita kwa kuzidi kuonyesha kasi kubwa ya utendaji kazi na kudumisha umoja na amani kwa maendeleo zaidi.

Rais Samia aliyasema hayo katika salamu zake za Mwaka Mpya 2023 kwa Watanzania kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu usiku wa kuamkia juzi.

"Pamoja na mafanikio, nitumie fursa hii kuwakumbusha viongozi wenzangu tuliobeba jukumu zito la kuhudumia Taifa hili, kwamba Watanzania wana matumani makubwa kwetu na tunatarajiwa kuendelea kuliongoza Taifa hili kwa juhudi, uadilifu na kwa misingi ya haki na sheria.


"Hapana shaka kwamba kila mwisho, unaanzisha mwanzo mpya, mwisho wa 2022 ndiyo mwanzo wa 2023. Hakuna anayeweza kuurudisha muda nyuma na akarekebisha yaliyoharibika, hivyo basi, tufanyie kazi sasa changamoto zilizotukwaza 2022," aliagiza.

Rais alisema ili kujenga mustakabali mzuri, mwaka mpya ni kitabu kisicho na maandishi wala kalamu, hivyo jukumu liko mikononi mwa kila mmoja, hivyo wakati huu, ni wa kuandika hadithi njema ya mafanikio ya baadaye.

"Tunapokusanyika pamoja na familia zetu, ninataka niwatakie nyote mwaka wenye afya njema, neema na furaha. Leo hii wapo wenye afya njema na furaha kutokana na sababu mbalimbali za mafanikio ya kimaisha.

"Lakini kama kawaida ya maisha, wapo wengine wanaopitia changamoto kadhaa. Pamoja na changamoto tulizopitia mwaka 2022, ninawaomba tusikate tamaa, bali changamoto zozote zile zitupe nguvu na tuutazame mwaka mpya kwa matumaini makubwa mbele yetu," alisema.

Rais Samia aliongeza: "Ni katika mustakabali na utamaduni huo wa kutokata tamaa ndiyo ndoto na matumaini ya Taifa letu, mwaka hadi mwaka. Ninatumia fursa hii kumwomba Mwenyezi Mungu mkarimu, atuondolee kila aina ya dhiki, atupe faraja na furaha; na awalaze mahali pema peponi wapendwa wetu wote waliokwisha kutangulia katika ufalme wa milele."

Rais alisema wakati mwaka 2022 ukikamilika, mshikamano umeendelea, akisema serikali itaendelea kufanya kila litalowezekana, ili mwaka huu uwe wa mafanikio makubwa zaidi.

"Wito wangu kwenu wananchi ni kuwa, tuendelee kushikamana, tuzidi kuupa nguvu umoja wetu, tutunze amani na utulivu wa nchi yetu, ili tuwe na maisha ya furaha na maendeleo ya juu zaidi.

"Ninawatakia kila la kheri, afya njema na mafanikio zaidi ya kiuchumi na kijamii kwa kila mmoja wetu na Taifa zima. Tuwe na mwaka mwema 2023," Rais Samia aliwasilisha.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo