Wema Sepetu achekelea kuukosa Ubunge

Na Nathaniel Limu, Singida
MSANII  maarufu wa tasnia ya filamu nchini, Wema Isaac Sepetu, ametangaza rasmi kuwa safari yake ya kuwatumikia wakazi wa mkoa wa Singida kupitia siasa, imeanza rasmi.
Wema ametangaza azima yake hiyo, muda mfupi baada ya kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa waombaji  wa ubunge viti maalum CCM mkoa wa Singida uliofanyika kwenye ukumbi mkubwa wa Kanisa la mjini hapa.
Wema ambaye alishiriki kwa mara ya kwanza katika kinyang’anyiro hicho alipata kura 90 na kushika nafasi ya nne kati ya waombaji 13, wakati Mbunge wa viti maalum kwa vipindi vitatu mfululizo , Diana Mkumbo Chilolo, aliapishwa baada ya kuwa mshindi wa tatu kwa kupata kura 182.
Msanii huyo ambaye alifanya vizuri katika kujinadi, alisema amejifunza mengi na kubaini mapungufu mbalimbali yaliyochangiwa na ugeni wake katika siasa,na kwamba  kuanzia sasa anajipanga vizuri, ili aweze kufanya vizuri zaidi kwenye safari yake ya kisiasa.
“Nitumie nafasi hii kuwashukuru wale  walionipa kura 90 na wale wote walioninyima kura kwa ujumla wao,wamenipa  hamasa na ari kubwa kuanza  rasmi safari yangu ya kisiasa, Ninachoomba ni Mungu aendelee kunipa uzima, ili siku moja ndoto yangu hii, iweze kutimia”,alisema Wema huku akitabasamu.
Awali mapema Wema alipofika Ofisi ya CCM mkoa, alikuwa kivutio kikubwa na kila mwana CCM alijitahidi kupiga picha naye huku wakisahau kambi zao za uchaguzi.
Alipoanza safari ya kuelekea ukumbi wa mikutano  wa Kanisa Katoliki mahali palipofanyikia mkutano wa uchaguzi, aliandamana na kikundi cha burudani cha Ikungi, na alishangiliwa na watu wengi waliojitokeza kando kando ya barabara  kwa ajili ya kumwona.
Aidha,aadhi ya wajumbe walidai kwamba kama kujinadi kwa mgombea ingekuwa sifa pekee ya mgombea kushinda ubunge wa viti maalum, Wema angepata angeshinda nafasi hiyo.
Wamedai kwamba Wema alijinadi vizuri, kwa ufasaha mkubwa na  kwa ufupi na kuvuta hisia za wajumbe ambao walishindwa kujizuia na kuvunja kanuni kwa kumpigia makofi msanii huyo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright 2025 EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo