Wasichana wawili wadogo waliachwa bila makao baada ya mama yao kuwakimbia punde kufuatia kifo cha baba yao.
Baba yao ambaye alikuwa ndiye wakutegemewa na familia hiyo alifariki dunia hospitalini baada ya kupata majeraha kufuatia ajali katika eneo lake la kazi.
Siku chache baada ya kumzika baba yao, madada hao kutoka Kavumu Avenue, Kiziba One katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, walisema mama yao aliondoka na hawajui aliko. "Mama yetu alipanga virago vyake na kwenda kana kwamba anaenda kazini, lakini hakurudi tena.
Hata hakutuaga ili kujua kwamba hatarudi. Tuliendelea kumsubiri tu arudi bila mafanikio. Siku zilipita wiki na miezi na ndipo tulipogundua kwamba alituacha kabisa, na ukutokuwa na uwezekano wa kurudi," Natalie, mmoja wa watoto hao aliambia Afrimax English.
Natalie na dada yake hawaendi shule, hawana chanzo cha mapato au jamaa wa kuwalea. Watoto hao wawili huwa wanarandaranda mitaani na wakibahatika wakati mwingine hupatana na msamaria mwema anayewasaidia na chakula.
Jirani mmoja aliguswa sana na hali ya watoto hao na kujaribu kuwalinda ili kuwasaidia kupata chakula. “Tunawafahamu watoto hawa kwa sababu sisi ni majirani na kila mara tunajaribu tuwezavyo kuwasaidia kwa vyovyote tuwezavyo,” Safari alisema.