Kilio wafuasi wa Nabii Seguye, waiomba Serikali kuwafungulia Kanisa lao

Baadhi ya waumini wa Kanisa la Word of Reconsiliation Ministry (WRM), linaloongozwa na Nabii Nicholaus Seguye wamesema wana imani na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan italifungulia kanisa hilo kufanya shughuli zake.


Wakizungumza, waumini hao wamesema hawadhani kwamba kanisa hilo limetenda kosa la jinai litakalofanya lisiruhusiwe kuhudumu maneno ya Mungu.

Sesilia Mbogwa mmoja wa waumini wa kanisa hilo aliliambia gazeti hili kuwa, kwa kipindi ambacho kanisa limefungwa, wamejisikia huzuni kwa kuwa wanakosa kufanya ibada ya kumuabudu Mungu.

“Hatujajua kwa undani jambo ambalo limefanya kanisa letu kufungiwa na serikali lakini tuna imani kwamba ni mambo yanayoweza kuzungumzika ili sisi waumini tuendelee kumuabudu Mungu,” alisema Sesilia.

Abiudi John yeye alisema anamuomba Rais Samia kuingilia kati jambo hilo kwa kuwa kazi iliyokuwa ikifanyika katika kanisa hilo licha ya kumuabudu Mungu, kiongozi wao Seguye alikuwa mmoja wa watu wanaohamasisha amani na mshikamano nchini.

“Nasema kutoka moyoni kwamba kama kuna kasoro zimejitokeza namuomba waziri husika, aone jinsi ya kuwaambia viongozi wetu jinsi ya kuzirekebisha ili huduma iendelee,” alishauri John.

Mmoja wa watendakazi wa kanisa hilo ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini alipozungumza na Ijumaa na kuomba jina lake lisiandikwe kwenye gazeti kwa kuwa sio msemaji alisema, tatizo hilo linashughulikiwa na viongozi wa kanisa ili huduma iendelee ya kumtukuza Mungu.

“Ninavyofahamu mimi ni kwamba tatizo hilo linashughulikiwa na viongozi wa kanisa na nina imani na serikali yetu kwamba muda si mrefu huduma itarudi,” alisema mtenda kazi huyo.

Huduma za kiroho katika Kanisa la The Word of Reconciliation Ministries (WRM) la Kivule- Matembele ya pili, jijini Dar es Salaam zimesitishwa huku ulinzi wa Jeshi la Polisi ukiimarishwa ili kuzuia huduma yoyote isifanyike.

Huduma ya kanisa hilo lililo chini ya Nabii Nicolaus Suguye imezuiliwa kwa zaidi ya wiki tatu zilizopita, huku waumini zaidi ya 4,000 wakidai kupewa maelekezo ya kutakiwa kutafuta maeneo mengine ya kuabudu.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema kwa sasa anayelalamikia si yeye (Suguye) kwani yeye anajua kwa nini amefungiwa.

Muliro alisema wao ni wasimamizi wa sheria na wanapaswa kuzilinda, “Na kama (kufungiwa) ingekuwa ni kinyume cha sheria au taratibu unafikiri wenye kanisa wangekaa kimya? Kuna vitu haviko sawa kuhusiana na taasisi hiyo ya dini na lazima vitimie.”

Suguye, anayetambuliwa na waumini wake kama nabii, alianza kutoa huduma za kiroho mwaka 1998 kabla ya kuanzisha kanisa hilo mwaka 2007.

Kanisa hilo limefungwa ikiwa ni mwaka mmoja baada ya wizara hiyo chini ya ofisi ya Msajili wa Jumuiya, Emmanuel Kihampa kutangaza mabadiliko ya hadhi ya vyeti vya usajili wa taasisi za kidini na jumuiya mbalimbali za kijamii inayoelekeza kuhuisha vyeti vya usajili kila baada ya miaka mitano.

Kisheria ili kusajili taasisi hizo za kidini, mwombaji anatakiwa kuwa na nakala za katiba, kujaza fomu mbili yenye wasifu wa viongozi, muhtasari wa vikao, kulipia ada ya maombi ya usajili, ada ya usajili, ada na tozo ya kila mwaka baada ya kusajiliwa na kuwasilisha ripoti ya utendaji na fedha ya kila mwaka, jambo ambalo wafuasi wa kanisa hilo wanasema haviwezi kushindikana.

Chanzo: gazeti la Ijumaa


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo