Wananchi wilayani Makete mkoani Njombe wametakiwa kuyafumbia macho matukio ya ukatili yanayojitokeza katika maeneo yao kwani kwa kufanya hivyo kwa kuwa zipo sheria zinazosimamia masuala hayo ili zifuatwe na haki itendeke
Hayo yamebainika Desemba 5, 2022 katika ufunguzi wa wiki ya msaada wa
kisheria tukio lililofanyika kiwilaya katika kijiji cha Kisinga kata ya
Lupalilo wilayani hapo kabla ya kufikia kilele chake Desemba 12, 2022
Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Mkurugenzi wa shirika la wasaidizi wa
Kisheria wilaya ya Makete (MAPAO) Mch. Denis Sinene amesema ni wakati sasa wa
jamii ya Makete kuacha kukaa kimya na badala yake waripoti pale wanapoona
vitendo vya ukatili vinapofanyika ili hatua ziweze kuchukuliwa
"Tujitokeze kutoa taarifa, vyombo saivi vipo salama, uongozi wa vijiji
vyenu upo,uongozi wa kata upo, nenda katoe taarifa, na nyie watoto tumewaita
hapa ukiona mtu anasema neno lisilofaa kamwambie mama, kamawambie baba, nenda
kamwambie kiongozi kwamba huyu nimeona ananishikashika sehemu ambazo sitaki,
sasa unakaona na kenyewe kanasema shika sana halafu na lizee lenyewe, mmesikia
nyie vijana wangu hapo" amesema Mkurugenzi Sinene
Amesema watu wanafanya matukio sio kwamba hayapo Makete, matukio yapo
lakini watu wanaficha uovu hivyo kijiji cha Kisinga kinatakiwa kubadilika na
kuwa mfano wa vijiji vingine vyote vya wilaya ya Makete
Kwa upande wake Mwanasheria wa halmashauri ya wilaya ya Makete Apollo
Laizer ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maandimisho hayo
amesema matukio yote ya ukatili yanayotokea katika jamii yaripotiwe kwenye
vyombo husika ikiwemo kwa jeshi la polisi kwa kuwa ukatili unapofanyika
hautakiwi kufichwa ndani ya jamii kwa madai ya kusuluhishwa
"Hata viongozi wa serikali ya kijiji msifichefiche masuala ya ukatili
yanayojitokeza na kujaribu kuyasuluhisha, hapana, yapelekwe mahala husika ili
haki itendeke kwa waathirika, matatizo mengine ya ukatili yanayojitokeza
yanapelekea msongo wa mawazo hata mara nyingine watu wengine kujitoa uhai, lakini
wanapopata haki wanapopata msaada wa kisheria msongo wa mawazo utaondoka na
wataweza kurudi katika jamii, lakini pia wale wanaotekeleza vitendo vya ukatili
ni lazima waadhibiwe kwa mujibu wa sheria" amesema Laizer
Amesema vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika katika jamii
ni vitendo vya jinai hivyo sio vitendo vya kusema watu wanakaa mezani na
kuyamaliza hivyo vinatakiwa kupelekwa katika vyombo husika ikiwemo kuvitolea
taarifa polisi katika dawati la jinsia na ikibidi vipelekwe mahakamani ili
mwisho wa siku kuwe na jamii inayozingatia utawala wa kisheria