Katika kuelekea kilele cha
kumbukumbu ya miaka 61 ya Uhuru, wilaya ya Makete mkoani Njombe imeendelea
kutekeleza shughuli mbalimbali za kijamii kwa kufuata muongozo uliotolewa na
ofisi ya Waziri mkuu ya namna maadhimisho hayo yatakavyofanyika kiwilaya
Leo Desemba 6,2022 watumishi
wa Halmashauri ya wilaya ya Makete wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaj na Katibu
Tawala wa Wilaya kwa kushirikiana na Taasisi za serikali na wananchi
wameshiriki kufanya usafi wa mazingira ya hospitali ya wilaya ya Makete pamoja
na kupanda miti katika eneo la kituo cha Polisi Makete
Baada ya kukamilika kwa
shughuli hizo, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete William
Makufwe amesema wamefanya usafi katika hospitali ya wilaya ya Makete kwa
kufyeka majani, kuchoma majani yaliyokauka, kutoa makopo, makaratasi na
takataka zote zisizotakiwa katika eneo la hospitali ikiwa ni utekelezaji wa
jukumu lililopangwa katika kuadhimisha miaka 61 ya uhuru
"Wiki hii matukio
yataendelea na mwisho wa siku tutahitimisha kwa hiyo tarehe 9, kwa hiyo usafi
uliofanyika hopsitali tunaamini kabisa umekuwa na manufaa na faida kubwa, kwaza
kwa mandhari yenyewe ya hospitali pamoja na wagonjwa wanaoendelea kupata huduma
pale, wito wangu tumefanya usafi kwenye hospitali ya wilaya kwa maana ya taasisi
moja tuliyoichagua kwa ajili ya usafi huo lakini maana yake nini, kila mtu
kwenye eneo lake, eneo la makazi, eneo la biashara, na maeneo mengine yote
lazima tudumishe usafi wa mazingira yetu" amesema Makufwe
Kuhusu zoezi la pili la
upandaji miti, Mkurugenzi huyo amesema wamepanda miti zaidi ya 700 kwa ajili ya
kutunza mazingira na kulinda mipaka ya kituo kikuu cha polisi wilaya ya Makete
"Tuliweka ratiba yetu
ya wiki hii na leo hii tarehe 6 mwezi wa 12 tulipanga tuwe na tukio la kupanda
miti kwa ajili ya kuenzi basi uhuru wetu wa miaka 61 ya uhuru wa Tanzania bara
kwa kupanda miti kama kielelezo cha utunzaji wa mazingira katika maeneo yetu,
sasa kwa ratiba tuliyoipanga tulipanga tupande miti katika eneo la kituo cha
polisi Makete, kituo kikuu cha polisi wilaya ya Makete, Kuna eneo ambalo lipo
hapa kubwa ambalo lote kwa maana ya kulinda mipaka ya kituo hiki tumepanda miti
zaidi ya 700na miti 700 hii tunatarajia kwa sababu Makete tuna hali ya hewa
nzuri mvua zinanyesha miti yote itapona" amesema Mkurugenzi Makufwe
Ametoa wito kwa wananchi
wanaoishi maeneo karibu na ilipopandwa miti hiyo waitunze miti hiyo na kuepuka
vitendo vya kuihujumu ikiwemo kuing'oa ama kuchungia mifugo itakayoiharibu miti
hiyo
Kwa upande wake Mkuu wa
Idara ya Uhifadhi wa Maliasili na Mazingira Wilaya ya Makete Upendo Mgaya
amewasihi wanamakete kwa ujumla kutumia vizuri mvua zilizoanza kunyesha
wilayani hapo kwa kupanda miti ya kutosha kwa maana ya kutunza mazingira na pia
kupanda miti inayostahili kupandwa kulingana na eneo kwa maana ya kutopanda
miti ya mbao kwenye mashamba ya kilimo ama miti ya mbao au ya kigeni kwenye
vyanzo vya maji
Joseph Mbilinyi ni
Mwenyekiti wa mtaa wa Dombwela ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mamlaka ya mji Mdogo
wa Iwawa ametoa rai kwa wakazi wa kitongoji cha Dombwela kilipo kituo hicho cha
polisi kutunza miti hiyo iliyopandwa na kujiepusha na vitendo vya kuiharibu
kupitia mifugo yao na kama hawajawahi kufanya kazi kijeshi, basi wale wote
watakaokamatwa wakipeleka mifugo eneo hilo wakati wa kiangazi adhabu yao itakuwa
kupanda miti wakati huo wa kiangazi mpaka ikue.