Serikali inatarajia kusaini mkataba na Mkandarasi atakayejenga barabara ya Makete Mbeya kipande cha Kitulo hadi Iniho cha urefu wa kilomita 36.3 kwa kiwango cha lami
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) imesema kuwa mkataba huo utasainiwa kesho Desemba 28,2022 katika ukumbi wa Madihani Villa Makete mjini
Ikumbukwe kuwa akiwa wilayani Makete Agosti 9,2022 wakati wa ufunguzi wa barabara ya Makete Njombe kwa kiwango cha lami, Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan alimtaka Waziri wa ujenzi na Uchukuzi kutoa majibu ya lini barabara ya Makete Mbeya itaanza kujengwa kwa lami ambapo alisema mkandarasi ataanza ujenzi Septemba 2022 lakini inategemewa mkandarasi kuanza kazi mara baada ya utiliaji saini huo wa Kesho Desemba 28,2022
Barabara ya Mbeya Makete imekuwa tegemezi kwa wananchi wa Makete hususani katika kusafirisha mazao ya biashara na chakula lakini pia kwa usafiri wa wakazi hao kwa kuwa ni kiunganishi cha mkoa wa Njombe na Mbeya na imekuwa ikisumbua hasa msimu wa mvua, hivyo kujengwa kwa kiwango cha lami kutakuwa mkombozi kwa wilaya hiyo.