Kijana ajiua Kukwepa deni la Sh. 45,000/=

KIJANA anayefahamika kwa jina la Bukindu Bukindu (22), mkazi wa kijiji cha Ihega, Kata ya Bukoli wilayani Geita amejiua kwa kunywa sumu ya panya, akihofia kudaiwa Sh 45,000 aliyoagizwa kununua soda.


Akizungumuzia tukio hilo, mama wa marehemu, Shija Anthony, amesema mwanaye alijiua siku ya sikukuu ya Krismasi, Desemba 25, 2022, ambapo alipatiwa fedha hizo na muuza duka kufuata vinywaji duka la jumla.

Amesema baada ya kufika duka la jumla alilipia na kukabidhiwa vinywaji na alipotaka kuondoka alizuiwa na kuamriwa kurejesha vinywaji na alipoeleza ameshalipia wahusika hawakumuelewa.

“Basi akaja kwa yule bosi wake aliyekuwa amemtuma, akaja kumueleza, ikabidi waende na yule bosi, walipofika kule wakaambiwa huyu mtoto hela ya vinywaji hajalipia.

“Yule bosi naye akamwambia, wewe dogo mimi nataka hela yangu, ukija dukani uje na hela, baadaye sasa wakati mimi napika akaniomba funguo, akatoka na kikombe cha maji, akaingia kwake akafunga,” amesema na kuongeza kuwa mwanawe alihitimu darasa la saba mwaka huu.

Ameeleza akiwa ndani mwanaye alikunywa sumu na kuanza kutapika na baada ya kubaini walifanya juhudi za kumpeleka zahanati kupata huduma ya kwanza, lakini hawakufanikiwa kuokoa uhai wake.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Ally Kitumbu amethibitisha tukio hilo na kueleza uchunguzi unaendelea kupata kiini halisi cha tukio hilo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo