Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imeielekeza ofisi ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora kwa niaba ya Kamishna wa Ustawii wa Jamii, kushirikiana na vyombo vya haki mkoani humo kuhakikisha wanafufua shauri la wazee waliochapwa viboko kwa tuhuma za kishirikina, ili mashahidi watoe ushahidi wao kuhusu kesi hiyo.
Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa na Waziri Dk Dorothy Gwajima, imeleza kuwa baada ya kesi hiyo kufika mahakamani, Wizara ilifuatilia na kugundua kesi hiyo iliondolewa baada ya walalamikaji na watuhumiwa kutoitikia wito wa mahakama.
Alisema video fupi inayosambazwa ikionesha malalamiko ya wazee hao kuchapwa viboko kwa tuhuma za uchawi, liliripotiwa Juni, 2022 na lilifikishwa mahakamani, lakini liliondolewa baada ya mahakama kutopewa ushirikiano na walalamikaji.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Gwajima ameeleza kulaani vitendo vya watu kuchukua sheria mkononi kwa kuhukumu wananchi kwa vipigo na kwamba atalifuatilia ili sharia ichukue nafasi kwa yeyote aliyehusika na jambo hilo.