Mwanaume mzee aliyekuwa na ujasiri wa hali ya juu, alihudhuria ibada katika kanisa la pasta Ezekiel Odero, lililoko Mavueni, Kaunti ya Kilifi na kumtaka amuombee ili apate mke.
Mzee huyo alisimulia kwa pasta Ezekiel jinsi alivyokuwa ameoa wake wanne awali, ila sasa yuko solemba.
Babu huyo alidokeza kwamba wake zake wawili wa kwanza walimtema, kisha akaoa wake wengine wawili walakini waliaga dunia na sasa anataka mke mwingine wa kuishi naye.
Mzee huyo alimuambia mwanzilishi wa Kanisa la New Life Christian:
"Sina mke sahii. Wanawake wamefika karibu nne, wawili walienda nikafanya tena wawili wakaufa. Sasa mimi niko tuu, nifanyaje?" "Unataka bibi mwengine?" Ezekiel, ambaye amemmuoa pasta Sarah aliuliza.
Ezekiel na waumini wa kanisa lake waliangua kicheko, kufuatia ombi la mwanamume huyo mzee.