Mwili wa mtoto uliokuwa umezuiliwa Muhimbili kisa Deni waachiwa

Mwili wa mtoto wa mwaka mmoja, Constantine John uliokuwa umezuiliwa kwa siku tatu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) baada ya ndugu kushindwa kulipia gharama za matibabu Sh2.1 milioni, umeachiwa.


Constantine ambaye alikuwa akitibiwa hospitalini hapo kwa takribani mwezi mmoja alifariki Desemba 14, 2022 kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kumwagiwa chai ya moto. Alilazwa katika wodi ya watoto mahututi (PICU) kwa siku 14.


Mwili huo uliotarajiwa kuzikwa Desemba 14, 2022 umeachiwa jana jioni baada ya ndugu kusota hospitalini hapo tangu asubuhi hadi jioni wakiuomba mwili huo.

Akizungumza kwa njia ya simu leo Desemba 17, 2022, Joel Lucas ambaye ni shemeji wa mama mzazi wa mtoto huyo, Bernadetha John, ameishukuru Mwananchi kwa juhudi ilizofanya kuhakikisha mwili wa mtoto huyo unaanchiwa.

“Nawashukuru sana, mmefanya kazi kubwa jana tulipewa mwili lakini muda ulikuwa umekwenda tukauacha, muda huu saa 3:32 asubuhi nipo hapa MNH tunauchukua mwili wa mtoto na tunakwenda kuuzika Mbezi,”amesema.

Lucas amesema haikuwa kazi rahisi mwili huo kuachiwa kwani Desemba 15, 2022 walikesha MNH tangu asubuhi hadi saa mbili usiku jambo lililowafanya wapoteze matumaini ya kuupata mwili huo.

Kuzuiwa kwa mwili

Lucas amesema baada mtoto huyo kupoteza maisha Desemba 14, 2022, wazazi wa mtoto huyo walitakiwa kulipia gharama ya Sh4.2 milioni zilizotumika kwenye matibabu siku zote alizokaa hospitalini hapo.

“Baada ya mtoto kupata changamoto, baba wa mtoto alimkimbia mwanamke, tulikwenda Idara ya Ustawi wa Jamii Hospitali ya MNH tukawaelezea hali yetu kwamba hatuwezi kumudu gharama hizo wakasema wamepunguza Sh2 milioni.

“Deni likabaki Sh2.1 milioni, sasa kwa kuwa yule kijana aliyempa mimba amekimbia ikabidi sisi tukajichanga tukapata Sh700,000 tukapeleka Ustawi wa Jamii ya Hospitali ya Muhimbili wakakataa wakasema wanataka ifike angalau Sh1 milioni,” amesema.

Akiwa Idara ya Ustawi wa Jamii ya MNH majira ya saa 2:20 asubuhi jana, Lucas amesema tangu Desemba 14, 2022 wanahangaika ili wapewe mwili huo huku wakipeleka nyaraka mbalimbali zikiwemo za serikali za mitaa kuonyesha binti huyo hana uwezo lakini wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa.

Jana, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano MNH Neema Mwangomo alikiri mwili wa mtoto huyo kuwepo hospitali hapo na kubainisha kuwa hospitali hiyo haijazuia mwili kwani kuna utaratibu lazima ufuatwe.

“Leo (jana) wamekamilisha tararibu wanachukua mwili wa mpendwa wao, bili ya awali ilikuwa ni Sh4.2 milioni, hospitali ikamsamehe takribani Sh2 milioni na kutakiwa kulipa Sh2.1 milioni na wamelipa Sh790, 000” alisema Mwangomo.

Alichowahi kusema Rais Samia

Wakati hilo likitokea, itakumbukwa kwamba Juni 2021, Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizungumza na wanawake jijini Dodoma, alikemea tabia ya hospitali kuzuia mwili akimuagiza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuhakikisha anaweka utaratibu wa kuondoa changamoto hiyo.

“Hata kidini tunaambiwa mtu asiende kuzikwa mpaka deni limelipwa, lakini si deni la serikali naomba muweke mpango mzuri, hapa nataka wananchi wanielewe, sio kwamba deni lisilipwe…kuwekwa mpango mzuri wa kulipa deni bila kuzuia maiti.

“Mpango mzuri ni kutoa gharama za matibabu wakati matibabu yanaendelea badala ya kusubiri siku ya mwisho mgonjwa amefariki unamwambia Sh3 milioni huku anafanya mpango namna gani? Taratibu za mazishi? Hii sio sawa, naomba muweke mpango mzuri wa kulishughulikia hili,” ameagiza Rais Samia.

Juni 2021, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi alisema tayari mwongozo na barua mbalimbali kuhusu suala hilo umetolewa kwa hospitali zote nchini.
Chanzo: Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo