Mpya za sasa hivi kuhusu Feisal Saul "Fei Toto"

SAKATA la kiungo wa Kimataifa wa Tanzania, Feisal Salum Abdallah na Yanga limechukua sura mpya kufuatia mchezaji huyo kuomba kuondoka na kulipa gharama za mkataba wake.


Taarifa ya Yanga leo imesema; “Klabu  inathibitisha kupokea barua kutoka kwa mchezaji tarehe 23 Disemba 2022 inayoeleza kuvunja Mkataba wake baina yake na Klabu.

Klabu ya Yanga imemuandikia na kumjibu Feisal na miongoni mwa majibu ni kama ifuatavyo;
Hakuna misingi ya kikanuni wala kisheria kulingana na mkataba wake ambazo zinampa haki mchezaji kusitisha mkataba wake na Klabu kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa sasa

Kanuni na Taratibu za FIFA ziko wazi na zimeelezea taratibu zote juu ya Jambo la aina hii.
Kwamba, Mkataba baina ya mchezaji na Klabu hauwezi kuvunjwa na upande mmoja tu bila kujadiliana na upande wa pili wakati msimu wa ligi ukiwa unaendelea.
Kwamba, kwa mazingira hayo, barua ya mchezaji ina dhana potofu na haina misingi ya kisheria ya kuvunja mkataba baina ya klabu na mchezaji
Na kwa mantiki hiyo, tumemuagiza Feisal, azingatie matakwa ya mkataba wake kama ilivyoelezwa katika mkataba huo.

Klabu pia imemkumbusha Feisal, mkataba wake wa sasa ni halali hadi ifikapo Tarehe 30 Mei 2024
Pamoja na hayo, tunapenda kuujulisha umma kuwa, kwa kuthamini kiwango na mchango wa Faisal kwa klabu yetu, tayari tulishaanza mazunguzo baina ya klabu ya Yanga na wawakilishi wa Feisal wakiongozwa na mama mzazi wa mchezaji ili kuboresha maslahi yake na kuongeza muda wa mkataba wake wa sasa ambao unaishia Mei 2024.

Hata hivo, Klabu haijapokea majibu mbadala wa mapendekezo ya maboresho haya kutoka upande wa Feisal na wawakilishi wake na badala yake tumepokea barua inayoelezea kuvunja mkataba kutoka upande wa Feisal ambayo ni Kinyume na makubaliano ya mkataba wake wa sasa.

Klabu tayari imesharejesha fedha kiasi cha TZS 112,000,000 (Millioni Mia Moja na Kumi na mbili) ambazo Feisal aliziweka katika Akaunti za Klabu.
Tunapenda kueleza kuwa, kuna taratibu na kanuni za Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) na zile za Shirikisho la Mpira wa miguu Duniani (FIFA) ambazo ni lazima zifuatwe na timu yoyote ile inayotaka kumsajli mchezaji yeyote wa Klabu ya Young Africans SC (YANGA).

Yanga, inasisitiza kuwa, Feisal Salum Abdallah ni mchezaji halali ya Yanga na ana mkataba hadi kufikia Mei 30, 2024,” imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Idara ya Habari ya Young Africans Sports Club kupitia app ya klabu hiyo.
Taarifa zisizo rasmi zinasema Fei atajiunga na klabu ya Azam FC kwa mkataba wa miaka mitatu na tayari amekwishaondoka kwenye kambi ya Yanga.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo