Mlinzi wa usiku ameuawa kwa kukatwakatwa katika tukio la ujambazi lililofanyika katika Kanisa la Redeemed Gospel lililopo Nguluni Tala katika Kaunti ya Machakos, Kenya
Aidha, genge hilo la ujambazi lilipora vifaa kadhaa vya kielektroniki vyenye thamani ya Sh 500,000 baada ya kuingia ndani ya uzio wa kanisa yapata saa 8 usiku.
Kwa mujibu wa polisi, watu hao kwanza walimfunga mlinzi mmoja wa waliokuwa zamu kisha wakaelekea katika ofisi kuu walikopanga kupora mali.
Taarifa zinasema huko walikutana na upinzani kutoka kwa mlinzi mwingine, Feminus Makau (58) aliyekuwa akilinda mahali hapo ndipo walipomshambulia na kumuua kwa kumkata kichwa kisha wakautoa mwili wake nje na kuutelekeza.
Ilielezwa kuwa, muda wote huo mmoja wa majambazi hao alikuwa akimlinda mlinzi mwingine ambaye alikuwa amefungiwa ndani ya chumba.
Baada ya kukamilisha uhalifu huo, wavamizi hao walitoroka kupitia ukuta wa pembeni wakitelekeza baadhi ya mali walizokuwa wamepora katika ofisi ya kanisa.
Polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili huo hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Walisema wanamhoji mshukiwa wa shambulio hilo na msako wa kuwasaka washukiwa wengine unaendelea.
Katika tukio lingine; huko Ruaraka, mwanamke mmoja alichomwa kisu katika tukio la wizi na kufariki dunia baada ya kukaidi agizo la genge hilo la kusalimisha vitu vyake vya thamani na fedha taslimu na kusababisha kushambuliwa kwa kisu.
Mkuu wa Polisi wa Nairobi, Adamson Bunge, alisema wanatafuta genge lililohusika na tukio hilo.