Mzazi wa Mtaa wa Mlombo uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Babati mkoani Manyara Sophia Bakari(36) amewalalamikia wauguzi wa Hospitali ya Mji wa Babati Mrara kwa kushindwa kumhudumia vizuri alipoenda kujifungua usiku wa kuamkia Desemba 17.
Alitoa malalamiko yake leo Desemba 19 wakati akizungumza na Nipashe nyumbani kwake.
Sophia amesema alifika Hospitalini hapo majira ya saa 5:00 usiku akiwa na uchungu na aliwakuta manesi wawili alipotaka kupata huduma aliambiwa akae nje wapo wanakula kwanza.
Aidha baada ya muda mfupi aliambiwa aingie wodi ya wazazi akachague kitanda alale alifanya hivyo na uchungu ulipozidi aliwaambia manesi ila walikaidi kumhudumia.
"Nilipoona hawaji kunihudumia waliniambia niende Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara nilikataa nikasema uchungu umechanganya niliingia chumba cha kujifungulia alinifuata dada yangu ndio alinisaidia,"amesema Sophia
Amesema licha ya kumwambia aende kujifungulia Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Manyara ila hawakuangalia hata kadi yake ya kliniki kusoma historia yake huko nyuma.
Amesema kitu kilichomshangaza ni manesi wale wawili kumwambia dada yake kuwa anajifanya mjuaji anajua kuzalisha wajawazito na anafurahia kuchungulia maumbile ya wanawake wenzake.
Mama huyo aliyejifungua mtoto wa kike alisema baada ya kujifungua aliambiwa na manesi hao kuwa wamuuzie soksi ila aliwaambia kuwa anazo.
"Wale manesi wawili waliniambia nisisukume nifumbe mdomo na walisema wee sukuma tutaona ni nani atakuja kusaidia,"amesema.
Naye Hamis Katuga (65) ambaye ni mume wa Sophia alisema mke wake alikataliwa toka mwanzo na hospitali hiyo kuwa asipate huduma ya kliniki hivyo alikuwa anapata huduma hiyo katika Zahanati ya Mission.
Amesema alishangazwa na daktari wa zamu na wauguzi hao kumpa rufani mke wake bila kumpima japo aligoma kwenda.
Katuga amesema wodini hapo alishuhudia mwanamke mmoja akilalamika kupigwa makofi na nesi huku akimwambia anadeka hivyo aende hospitali ya rufani ya mkoa wa Manyara ambapo alikuwa anampigia simu ndugu yake aje amsaidie.
Kwa upande wake mganga mkuu wa hospitali hiyo Dk. Halima Mangiri amekiri kupokea malalamiko ya mgonjwa huyo ambaye alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 Desemba 17.
Dk. Mangiri amesema wameanza kufanya uchunguzi watakapobaini waliofanya makosa watawachukulia hatua za kinidhamu.
Chanzo: Nipashe