Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabiri Makame ameagiza TAKUKURU Wilaya ya Gairo kufanya Uchunguzi katika Mradi wa Ujenzi wa Nyumba ya Walimu Shule ya Sekondari Chagongwe kufuatia ziara aliyoifanya kukagua mradi huo na kubaini dosari kadhaa ikiwemo udanganyifu katika ununuzi wa Mbao ambapo Kamati ilinunua Mbao kwa Mzee Anold kwa gharama ya laki 8, na Mbao hizo kulipiwa tena zaidi ya milioni 4 kwa mzabuni ndg Flateri.
Kamati ilipoulizwa walikana kufanya biashara na Mzee huyo lakini walikiri kupokea Mbao kutoka kwake na walikiri kumlipa fedha shilingi laki 8, huku wakidai Mbao hizo aliagizwa na Mzabuni bwana Flateri kuleta Shuleni.
Kwa upande wake Mzee Anaold alikana kutomfahamu Mzabuni huyo na hajawahi kufanya naye biashara, na kwamba alieleza Mbao hizo aliagizwa na walimu wa Shule hiyo.
Pia Kamati imelipa shilingi laki 5 kwa ajili ya zabuni ya kuvuta Maji kutoka katika kisima kilichopo umbali wa Mita 100 kutoka eneo ambalo Jengo linajengwa, gharama ambayo ilitiliwa shaka.
Aidha, wamefanya udanganyifu katika ufyatuaji wa Tofali ambapo maelekezo yalikuwa Mfuko 1 wa Saruji utoe tofali 25, lakini mafundi walielekezwa kufyatua tofali zaidi ya 30 kwa Mfuko 1.
Fundi wa Tofali hizo bwana Elia John alikiri kwamba alipewa maelekezo hayo na Mkuu wa Shule, na Kamati walidai kwamba walifanya hivyo ili kupata tofali za ziada.
Baada ya upekuzi ilikamatwa mifuko 11 ya Saruji ikiwa imehifadhiwa Nyumbani kwa Mwalimu Ramadhani Mtiwa. Dosari zingine ni udanganyifu katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi ambapo kuna utofauti kati ya Vifaa vya Ujezni vilivyoagizwa na vile vilivyopokelewa.
Kufuatia Dosari hizo, Makame amemwagiza Kaimu Mkurugenzi Bi Msifwaki Haule kumvua Madaraka Mkuu wa Shule hiyo ndg Edga Mwihava, na kuwachukulia hatua wajumbe wote wa Kamati waliohusika kwa mujibu wa taratibu.
Aidha, ameagiza TAKUKURU Wilaya ya Gairo kufanya Uchunguzi wa kina na kuchukua hatua za kisheria.
Gairo imepokea fedha Tsh Mil 228 kujenga Nyumba za Walimu 4 zenye uwezo wa Kuchukua Kaya 8, katika Kata za Chagongwe, Idibo, Msingisi na Chanjale.