Watu watatu akiwemo mkazi wa Kijiji cha Mahaha wilayani Magu mkoani Mwanza, Zawadi Msagaja (20), wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumuua mtoto wake wa kike mwenye umri wa miezi sita kwa kumzika shambani akiwa hai ili wapate mali.
Ni kesi ya mauaji namba saba ya mwaka 2022 ambayo imesomwa na Mwendesha Mashtaka wa serikali Mwanahawa Changale, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Fortunatus Kubaja, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Mwanza ambapo amesema washtakiwa hao watatu akiwemo Zawadi Masaga ambae ni mama wa mtoto huyo, Elizabeth Kaswa ambae ni dada wa Zawadi pamoja na Mume wa Elizabeth ambae pia ni mganga wa kienyeji aitwaye Mussa Mazuri kwa pamoja walitenda kosa hilo Novemba 13 mwaka huu kinyume na kifungu namba 196 na 197 cha sheria ya kanuni ya adhabu marejeo namba 16 ya mwaka 2022.
Baada ya washtakiwa hao kusomewa shtaka hilo la mauaji linalowakabili, Hakimu Mkazi Mwandamizi Kubaja akaiahirisha kesi hiyo hadi kesho Desemba 28 itakapotajwa tena na washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo