Mtu amefariki dunia na wengine wanne wamejeruhiwa baada ya basi la kampuni ya AN Classic walilokuwa wakisafiria kutoka Tabora kwenda Mbeya kupata ajali katika eneo la Makongorosi wilayani Chunya mkoani Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Saimon Mayeka Saimon amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo leo Jumatano Desemba 7, 2022 na kwamba ilisababishwa na lori lililokuwa limebeba mitambo kulikwangua basi hilo pembeni.
“Ni kweli ajali imetokea kijiji cha Makongorosi, ambapo mtu mmoja amepoteza maisha papo hapo na wanne kujeruhiwa.
“Chanzo cha ajali kinaelezwa kuwa ni lori kukosa mwelekeo na kupita upande ambao sio sahihi na kupelekea madhara hayo,” amesema Mayeka.
Amesema majeruhi wa ajali hiyo walikimbizwa katika hosptali ya Wilaya ya Chunya na kwamba hakuna madhara mengine makubwa yaliyojitokeza.
“Taarifa za awali za maofisa wetu wa Polisi kitengo cha usalama barabarani nimeeleza chanzo cha ajali ni gari lililokuwa limebeba mitambo ambalo lilihama upande wake na kulivaa basi la abiria lililokuwa likitokea Tabora kuja Mbeya na kulikwangua pembeni,” amesema.
Mmoja wa abiria ambaye akuwa tayari kutaja jina lake, amesema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 2.30 za usiku ambayo ilisababishwa na uzembe wa roli lililokuwa likisafirisha mitambo ambapo dereva wake baada ya kusababisha ajali alikimbia.
“Tunaomba Serikali kuona namna ya kuboresha miundombinu ya barabara ambayo ni hatarishi kwa usalama wa abiria na mali zao na endapo mvua ingekuwa imenyesha watu wengi wangepoteza maisha,” amesema.
Chanzo: mwanachidigital