Abiria 57 wanusurika kifo ajali ya basi Morogoro


Abiria 57 waliokuwa wakisafiri kutoka Kilosa mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam na basi la Al El Saed wamenusurika kifo baada ya basi hilo kupinduka.


Ajali hiyo imetokea leo Jumatano Desemba 28 asubuhi katika barabara kuu ya Pwani-Morogoro na kusababisha abiria 16 kupata majeraha madogo ambao walipatiwa huduma ya kwanza na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoji huku kondakta wa basi hilo akikipelekwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro kwa matibabu zaidi.

Akizungumza eneo la tukio, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Morogoro, Sauda Mohamed amesema basi la Al El Saed lilikuwa likitokea wilayani Kilosa kwenda Dar es Salaam likiwa na abiria 57 na ilipofika eneo la Kitungwa lilipinduka wakati dereva wake akilikwepa basi la kampuni ya Allys iliyokuwa ikiyapita magari mengine likitokea Dar es Salaam kwenda Mwanza.

Mohamed amesema baada ya kutokea kwa ajali hiyo askari wa jeshi la polisi, jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika eneo hilo na kutoa huduma ya kwanza kwa abiria mali yao ambao wamepata majereha madogomaodogo lakini kufanya jitihada ya kuwasilana na uongozi wa basi la Al El Sael ili kupata basi lingine ili abiria kuendelea na safari yao.

“Basi hili la Al El Saed lilikuwa likitokea Kilosa kwenda Dar es Salaam ikiwa na abiria 57 lakini ilipofika eneo la Kitungwa Kingolwira Manispaa ya Morogoro dereva wake aliliangusha basi upande wake wa kushoto na kupinduka wakati akikwepa kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya mabasi ya Allys iliyokuwa ikitoka Dar es Salaam kuelekea Mwanza na tayari tunamzuia dereva wa basi la Allys kwa kuhusika katika ajali hii.” amesema Mohamed

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Morogoro, Emmanuel Ochieng amesema askari wa jeshi hilo walifika kwa wakati eneo la tukio na kutoa huduma ya kwanza kwa abiria 16 ambao wamepata majereha mepesi.

“Baada ya kufika eneo la tukio abiria 16 tumewapatia huduma ya kwanza kwa kuwatibia majereha madogo madogo isipokuwa kondakta wa basi la Al El Saed yeye amekimbizwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro kwa huduma zaidi kwani ndiye aliyepata majeraha makubwa.”amesema Ochieng.

Kwa upande wa abiria walionusurika ajali hiyo wamesema walipata mstuko uliosababishwa na mtingishiko ndani ya basi huku kukiwa na kelele kwa abiria wenzao na kuja kugundua kuwa tayari wamepata ajali.

“Nililala huku nikiwa nimemkumbatia mtoto mchanga katika kiti niliona mtingishiko na kuja kugundua basi letu limeanguka chini na wenzangu wakivunja kioo cha mbele na abiria wote tumetokea hapo mbele kutoka ndani ya basi baada ya kupinduka.”amesema Khadija Seleman.

Shuhuda alityeshuhudia ajali hiyo, Ally Juma amesema alikuwa alikuwa akiendesha baiskeli na baada ya kupita daraja la kwenda Kasi alishuhudia tukio hilo mbele yake.

“Ni uzembe uliofanywa na yule dereva wa basi la Allys kwani alikuwa akiyapita magari mengine eneo ambalo sio sahihi na dereva wa basi la Al El Saed kuona anaweza kugongana naye uso kwa uso akalazimika mkwepe lakini kumbe pembeni alikozidi ndio kulikosababisha basi kupinduka.”amesema Juma.
Chanzo:mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo