Jumla ya shilingi bilioni 69.754 zitatumika kujenga barabara ya Isyonje -
Kikondo - Makete kipande cha Kitulo - Iniho chenye urefu wa Kilomita 36.3 kwa
kiwango cha lami na Zege
Hayo yameelezwa leo Desemba 28, 2022 katika hafla ya utiliaji saini mkataba
wa ujenzi wa barabara hiyo baina ya Mkandarasi na Serikali iliyofanyika
Wilayani Makete mkoani Njombe
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa ameanza kwa kueleza ni
kwa nini mradi huo umechelewa kuanza ilihali wakati Rais Dkt Samia Suluhu
Hassan alipofika wilayani Makete kuzindua Barabara ya Makete NJombe ilielezwa
kuwa mkandarasi ataanza ujenzi Septemba 2022 akisema gharama za ujenzi wa
barabara kwa Makete ni kubwa kuliko maeneo mengine, pamoja na wakandarasi
kuomba zabuni kwa gharama kubwa, ni miongoni mwa vilivyochangia ujenzi huo
kuchelewa
“Mkandarasi huyu hajawahi kufanya kazi Tanzania mimi kama waziri siwezi
kufanya jambo, siwezi kucheza kamari na pesa za serikali, lazima nifanye kitu
sahihi kwa maslahi ya watanzania, tukaamua sasa tuwapeleke wataalamu wetu kuona
kazi ambazo mkandarasi huyu amefanya, tukatoa watu wa kwenda Srilanka na timu
moja ikaenda Kenya kuangalia au kufanya uhakiki kazi ambazo mkandarasi huyu
amezifanya” amesema Waziri Prof. Mbarawa
Waziri Mbarawa ameagiza Wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha
wanamsimamia mkandarasi huyo ili barabara hiyo ijengwe kwa wakati na kwa
viwango walivyokubaliana ili thamani ya fedha ionekane
“Naagiza TANROADS kusimamia mradi huu kwa udhibiti mkubwa ili barabara
iweze kujengwa kwa viwango vya juu kulingana na mkataba na hatimaye iweze
kudumu kwa muda mrefu kama ilivyosanifiwa, vile vile napenda kutoa shukrani
zangu za dhati kwa wananchi kwanza wa wilaya hii ya makete mkoa wa Njombe,
naomba sana tumpe ushirikiano mkubwa mkandarasi wetu, pia naomba sisi wenyewe
tuwe walinzi kuhakikisha kwamba vifaa vya mkandarasi tunavilinda vizuri na
kusiwe na uharibifu wa vifaa hivyo ili viweze kutumika vizuri na kazi iweze
kufanyika vizuri na kwa haraka zaidi, ninaamini tukifanya hivyo mradi huu utetekelezwa
kwa muda mfupi na tutaweza kuitumia barabara hii vizuri” amesema Waziri Mbarawa
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mhandisi Rogatus Mativila amesema
barabara hiyo itajengwa kwa kiashi cha shilingi Bilioni 69.754 ambapo barabara
hiyo itahusisha kiwango cha lami pamoja na zege katika baadhi ya maeneo ikiwemo
mlima wa Ipelele na mradi huo hadi kukamilika kwake utachukua miezi 36
Mhandisi huyo amesema katika ujenzi huo pia serikali imesamehe kodi ya
ongezeko la thamani yaani (VAT) ya shilingi Bilioni 12.113
“Zabuni za ujenzi wa barabara hii zilitangazwa tarehe 8 Machi 2022
Mkandarasi aliyepatikana ni kutoka kampuni ya China kwa gharama ya shilingi
bilioni 69.754 bila kuhusisha kodi ya ongezeko la thamani yaani serikali
imesamehe VAT ya shilingi bilioni kumi na mbili milioni mia moja kumi na tatu
laki moja arobaini na moja na miasaba ishirini na saba nukta tano moja, muda wa
utekelezaji wa mradi ni miezi 36” amesema Mhandisi Mtivila
Festo Sanga ni mbunge wa jimbo la Makete ameishukuru serikali kwa kusikia
kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Makete hivyo kujengwa kwa barabara hiyo
kutafungua uchumi wa wilaya hiyo na wananchi wake kwa ujumla
“Barabara hii ndiyo kiini cha uchumi wa wilaya ya Makete, hawa wanamakete
unaowaona hapa shughuli zao nyingi zipo Makete, robo ya population (idadi ya
watu) ya Makete, robo ya watu waliopo Mbeya, robo ya watu waliopo Tunduma,Songwe
ni wanamakete ambao watatumia barabara hii, barabara hii mtu alikuwa na uwezo
wa kusafiri kwa siku nne analala njiani lakini kwa wafanyabiashara mitaji yao
mingi imefia kwenye barabara hii, kuna magari mengi yameishia kwenye barabara
hii, kuna watu wengi wamefariki kwenye barabara hii leo ninasimama kama mbunge
wa jimbo la Makete, hii ni kete huu ni ushindi, ushindi kwa jimbo la Makete,
kwa sababu mheshimiwa Rais ametuheshimisha kwa kujenga barabara hii kwa kiwango
cha lami” amesema Mbunge Sanga
Naye mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Njombe Deo Sanga(Mb)
licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha za ujenzi wa
barabara hiyo, ametoa rai kwa wananchi kuwa walinzi na kujiepusha na wizi wa
vifaa vya mkandarasi anayetekeleza mradi huo
Alimivu Sanga ni mkazi wa kijiji cha Ipelele amefika kuhsuhudia zoezi la
utiliaji saini Mkataba huo na hapa akizungumza na mwandishi wetu amesema anaona
uchumi wa wilaya ya Makete na wananchi wake ukiende kukua zaidi kwa kuwa
watapata fursa ya kusafirisha mazao yao kwa wingi misimu yote pasina kukwama.