Jumla ya watoto 156,997 Wanatarajiwa kupatiwa chanjo ya polio awamu ya nne kwa siku nne mkoani Njombe ili kuwanusuru watoto na ugonjwa huo ulioripotiwa katika nchi jirani ya Malawi.
Kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Njombe, Katibu Tawala mkoa Judica Omary wakati akizungumza na vyombo vya habari amesema walengwa wa chanjo hiyo ni watoto wa chini ya umri wa miaka mitano bila kujali kama walipatiwa au laa.
Ugonjwa wa polio unasababishwa na kula au kunywa kinywaji chenye kinyesi chenye kimelea cha ugonjwa wa polio kwa mujibu wa wataalam wa afya.
Mratibu wa Chanjo mkoa wa Njombe Valeliana Makasi amesema jamii inapaswa kutoa ushirikiano wa dhati kwa wataalamu wa afya pindi watakapokuwa wakitoa chanjo hiyo ili kuwakinga watoto na ugonjwa huo ambao hauna tiba.
Baadhi ya wakazi wa Njombe, Husna Masudy na Agrey Kayombo wamesema serikali imechukua hatua stahiki za kuwakinga watu wake na hivyo watawapa ushirikiano wa kutosha.
Februari 17 mwaka 2022 kuliripotiwa kisa cha mgonjwa wa polio nchini Malawi na kusababisha Tanzania kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na janga hilo kwa kutoa chanjo kwa watoto.