Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ameungana na vijana wa mkoa wa Lindi kufanya usafi maeneo mbalimbali ya mkoa huo ikiwa ni maandalizi ya kumpokea Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye atawasili mkoani humo kesho Desemba Mosi, 2022.
Vijana hao walifanya zoezi hilo la kusafisha barabara baada ya kumaliza matembezi maalum katika maeneo mbalimbali ambapo walitumia fursa hiyo kufikisha salamu zao kwa Rais Samia kupitia kwa Waziri wa Habari Nape.
"Sisi Vijana wa Lindi ilifikia hatua baadhi ya wanasiasa walituita watoto tuliotengwa lakini walisahau licha ya mkoa wa Lindi kutotembelewa na Rais kwa muda mrefu Mama yetu Samia Suluhu akiwa Makamu wa Rais alitutembelea sana" Amesema Mustafa Dumbo kwa niaba ya vijana wa Lindi
Akiwajibu vijana hao Waziri Nape Nnauye amewataka vijana hao kutambua Rais Samia anaupenda sana mkoa wa Lindi na ndiyo maana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, anatokea huko.