Wakuta mifupa ya Binadamu wakichimba msingi wa jengo la Shule

Wafanyakazi wa mjengo wanaojenga madarasa mawili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi ya Voi, Kaunti ya Taita-Taveta wamegundua kaburi la halaiki katika shule hiyo.


Kwa mujibu wa Kenya News Agency, wafanyikazi hao, waligundua kaburi la halaiki la maelfu ya wanajeshi Waafrika mnamo Ijumaa, Novemba 11, ambao waliangamia katika Vita vya Kwanza vya Dunia vya mwaka wa 1914-1918.


Wafanyikazi hao wa ujenzi waligundua mifupa kadhaa ya binadamu, bangili, pete na pingu kati ya uvumbuzi mwingine adimu. Likithibitisha kisa hicho, shirika lisilo la kiserikali la Tsavo Heritage linaloshughulika na ukarabati na uhifadhi wa jumla wa Mfumo wa Ikolojia wa Tsavo na Maeneo ya Usambazaji, ilithibitisha kuwa Shule ya Msingi ya Voi imejengwa kwenye kambi ya zamani ya wabebaji mzigo eneo la Voi.


"Wakati wa uchimbaji wa darasa jana walipata kaburi la halaiki la maiti, mifupa na minyororo," Tsavo Heritage ilithibitisha ikionyesha kuwa eneo hilo halikushughulikiwa vyema na huenda lilikuwa na mifupa zaidi ndani. 


Ugunduzi huo ulizua furaha miongoni mwa wanahistoria na watafiti wa kitamaduni ambao kwa miaka mingi wamefanya kazi bure wakifanya utafiti wa hatima ya wapiganaji na wabeba mizigo wenye asili ya Kiafrika walioshiriki katika Vita vya Kwanza vya Dunia.


Kuna taarifa finyu kuhusu mahali walikozikwa wapiganaji wa WW1 huku masimulizi mengi kutoka kwa vita hivyo yakionyesha kwamba miili ya Waafrika iliachwa tu popote ilipoanguka; iwe vichakani au kwenye uwanja wa vita ulio wazi. 


Commonwealth War Graves, ambalo ni shirika la kimataifa linalowaheshimu na kuwajali wanaume na wanawake wa Jumuiya ya Madola waliofariki dunia katika Vita vya Kwanza vya Dunia na vya pili, liliishukuru Tsavo Heritage kwa kuwafahamisha mambo adimu yaliyopatikana.

Chanzo: TUKO.co.ke 


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo