Ndege ya Air Tanzania yashindwa kutua Bukoba

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mussa Mbura amesema sababu ya ndege ya ATCL kushindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba ni mvua mkubwa na ukungu uliokuwa umetanda katika eneo hilo.
 


Amesema ndege hiyo iliyotakiwa kutua leo saa 12:05 mchana, ilikumbana na changamoto hiyo ya hali mbaya ya hewa kiasi cha kumlazimu rubani kwenda kutua katika uwanja wa ndege wa Mwanza.


Ameongeza ndege hiyo ilikuwa mbali kwamba haijaanza kutua pindi rubani alipoamua kuchukua hatua hiyo.


Hata hivyo, amesisitiza kuwa ni ndege hiyo pekee ilishindwa kutua na kuongeza kuwa sasa hali ni shwari na ndege zinaendelea kutua hivyo hakuna ndege iliyozuiliwa kutua katika uwanja huo.


Kauli hiyo ya TAA imekuja saa chache baada ya Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Lugangira kueleza kwamba ndege aliyoipanda leo imeshindwa kutua katika uwanja huo wa Bukoba.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Mbunge huyo ameandika “Still shaken lakini Mungu ni Mwema. Nimepanda ndege asubuhi ya leo kwenda Bukoba. Safari ilikuwa na changamoto, tumefika lakini ndege ikashindwa kutua. Nampongeza Rubani kwa uamuzi sahihi wa kurudi Mwanza na sasa narudi Dar. Serikali ibebe kwa uzito suala la airport mpya Bukoba.”


Alipoulizwa kwa simu leo Alhamisi Novemba 17 kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA), Hamza Johari amethibitisha tukio hilo.


“Ni kweli nimepata taarifa ndege ya Air Tanzania imeshindwa kutua kutokana na hali mbaya ya hewa, kulikuwa na ukungu, mvua, radi na giza uwanja ukawa hauonekani, kwa hiyo rubani akafuta safari na kurudi Mwanza na ametua salama,” amesema.


Hali hiyo imejitokeza zikiwa zimepita siku 11 tangu ndege ya shirika la Precision ilipoanguka katika ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine 24 kuokolewa.


Via Mwanahalisi & Mwananchi


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo