Mtaa wa mabanda wa Githurai viungani mwa jiji kuu la Nairobi kulishuhudiwa kisanga baada ya mwanadada mmoja kuingia katika kanisa moja kwa fujo huku akidai kwamba mhubiri wa kanisa hilo alimlaghai pesa zake.
Mwanamke huyo alisikika akilalama kwamba mchungaji wa kanisa hilo alimlaghai kiasi cha laki 4 pesa za benki kuu ya Kenya.
Mwanamke huyo ambaye jina lake halijafahamika, alionekana kukasirika, alienda kanisani wakati ibada katika Kanisa la Rhema Gospel Church ikiendelea na kukatiza ibada.
Katika video iliyosambaa mtandaoni, mwanamke huyo wa Kenya ambaye alisema alikuwa anafanya kazi Saudi Arabia alidai kuwa mtu wa Mungu alimlaghai pesa zake zote alizochuma kwa bidii kutoka Saudia kwa njia ambazo hakutaja.
Alisema kwamba mchungaji huyo alikuwa amejificha na kuwa amekuwa akimtafuta kwa miezi ipatayo mitatu pasi na mafanikio yoyote na ndio maana akaamua kumfuata mbele ya waumini na madhabahu.
“Nimekuja huku nataka pesa zangu, ameniibia pesa zangu nilikuwa nafanya kazi Saudia. Anajificha kwa nini, ajitokeze aniletee pesa zangu, nimemtafuta miezi mitatu. Hakuna kuongea, ajilete yeye hapa. Aliniibia akiwa hapa kwa madhabahu, alinidanganya akiwa hapa. Mimi ninaogopa Mungu, kwa nini alinifanyia hivyo?” mwanadada huyo alisikika akisema kwa sauti ya juu huku akitaja jina la mchungaji huyo.
Kulingana na mwanadada huyo ambaye hakutaka kumsikiliza mtu yeyote mpaka aonane na mchungaji huyo, alisema kwamba alimtumia mchungaji pesa zake na kuzidi kuiapiza kanisa hiyo kuwa wamelaaniwa huku akilia kwa uchungu kuwa alipitia maisha magumu kupata pesa hizo ambazo mtumishi wa Mungu alikuja kumlaghai.
“Rehema Gospel Church Githurai Kimbo, nilimtumia pesa zangu nikiwa Saudia, mnajua uchungu wa kufanya kazi kwa Mwarabu nyinyi. Nyinyi mmelaaniwa mnakula jasho langu. Watoto wangu wanalala njaa,” mwanadada huyo alilia kwa uchungu.
