Esther Kaio wa Igembe Kaskazini, Kaunti ya Meru Kenya amepatwa na hatia ya kujaribu kumuua mumewe, kwa kumnyofoa sehemu zake nyeti.
Kwa mujibu wa ripoti ya Nation, Hakimu mkuu wa Maua Tito Gesora alimhukumu Esther kifungo cha miaka 15 jela baada ya kumvamia mumewe mnamo Novemba 19, 2021
Wakati akijitetea, mama huyo wa watoto watano alidai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili, na hivyo hakumshambulia mumewe kimakusudi. Esther aliishangaza mahakama baada ya kudai alijikuta amezuliwa na polisi, pasi na kujua makosa aliyokuwa amefanya.
Hata hivyo, kwenye uamuzi wake, hakimu huyo alisema kuna ushahidi unaothibitisha mwanamke huyo alikuwa na matatizo ya kiakili, ila matendo yake yanaashiria alifanya kitendo hicho kimakusudi. Upande wa mashtaka ulisimulia jinsi Esther alivyomshambulia mumewe akiwa amelala, baada ya kukataa kugawanya shamba la miraa. Akitoa ushahidi wake, mwanamume huyo alikumbuka jinsi mkewe alivyomshambulia kwa panga saa tisa usiku kabla ya kuchukua kisu na kukata sehemu zake nyeti.
Mkulima huyo wa miraa wa miaka 60 alipatikana amezirai, huku mwanamke huyo akijaribu kumwekea kemikali mdomoni mwake. Mahakama iliambiwa kwamba binti yake alisikia mfarakano na kuanza kupiga kamsa, ndipo majirani wakaja kumnsuru na kumpeleka babake katika Hospitali ya Misheni ya Chaaria.